Kamandi ya Nchi Kavu

KAMANDI YA JESHI LA NCHI KAVU

Kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu

Kuundwa kwake kumekuja miaka 43 baada ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanzishwa mwaka 1964.

Hii imekuwa ni historia katika kuleta mageuzi ndani ya Jeshi kwa kuliweka katika muundo utakaoleta ufanisi na tija zaidi katika Ulinzi na Usalama wa Taifa. Aidha, tukio hilo la kuanzishwa kwa Kamandi hii ni tukio la kihistoria la maendeleo ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

Kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kumetokana na dhamira safi ya Viongozi wa Serikali na Makamanda kuona umuhimu wa kuwa na Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ili kusimamia majukumu ya kiutendaji na kiutawala. Kwa sasa Makao Makuu ya Jeshi yamebakia na majukumu ya mipango na uamrishaji pekee.

“Leo ni siku muhimu kwani tunashuhudia mabadiliko ya muundo wa Jeshi letu ambalo sasa litaundwa na Kamandi tatu yaani Kamandi ya Wanamaji, Anga na Nchi Kavu”. Maneno hayo yalisemwa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete tarehe 4 Machi 2009, alipokuwa akizindua rasmi Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu mbele ya maafisa, wapiganaji na wananchi.

Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ina kazi ya msingi ya kusimamia utendaji wa kila siku wa Vikosi,Shule na Vyuo vilivyo chini ya Kamandi hiyo. Kamandi pia inaongoza vikosi vyote vya mizinga na vifaru, vikosi vya wahandisi wa medani pamoja na vyuo na shule zinazotoa mafunzo ya Kijeshi. Muundo wa Kamandi hii unabakia kuwa wa Kimataifa kwa vile umezingatia viwango vyote vya msingi katika kuanzisha Kamandi na kusimamia majukumu yake ya kimkakati na kisera wakati wa utendaji kazi.

Mara baada ya kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tarehe 01 Septemba, 1964 vikosi vya nchi kavu vilianza jukumu la kufundisha wapigania uhuru na hatimaye nchi mbalimbali zilikombolewa kutoka kwa serikali dhalimu za kikoloni. Nchi kama vile Msumbiji, Zimbabwe, Afrika ya Kusini, Angola na Namibia zilinufaika na msaada uliokuwa ukitolewa na JWTZ. Baadaye Jeshi la Nchi Kavu lilipata jukumu la kuendesha na kusimamia Operesheni ‘SAFISHA’ nchini Msumbiji wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1986 na 1988.

Ulinzi na Usalama wa Tanzania ni jukumu la kila raia, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alihimiza hilo mara kwa mara ambapo Jeshi lilitekeleza sera hiyo kwa kutoa mafunzo ya mgambo na kuyasimamia kikamilifu.

Mafunzo ya mgambo mpaka leo hii yanamuitikio mkubwa wa wananchi kwani hujiandikisha na kufanya mafunzo kwa hiari.

Mafunzo hayo yamebaki kuwa ni sehemu muhimu ya Jeshi la Nchi Kavu hadi Jeshi linapotimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Katika Vita ya Kagera 1978/79 Jeshi la Nchi Kavu lilinufaika kwa kuwajumuisha wanamgambo ambao walipigana bega kwa bega na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, kwani wote kwa pamoja walisonga mbele kukabiliana na majeshi ya Nduli Iddi Amin kwa kusaidiana na Vikosi vya Ulinzi wa Anga na Wanamaji, hatimaye kuikomboa ardhi ya Tanzania na kufanikiwa kuuondoa utawala dhalimu wa Idd Amin nchini Uganda.

Baada ya vita Serikali ya nchi hiyo iliomba baadhi ya Wanajeshi wa Tanzania wabakie na kutoa mafunzo kwa Jeshi la nchi hiyo. Vikosi vya Nchi Kavu pia vimetoa mchango mkubwa wakati wa maafa na katika ulinzi wa amani duniani kwa kushiriki katika operesheni nchini Liberia, Lebanon, Comoro, Sudan katika jimbo la Darfur na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Kihistoria, majukumu na kazi zote za Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ilizonazo sasa, zilikuwa zinatekelezwa chini ya Makao Makuu ya Jeshi. Makao Makuu ya Jeshi kupitia Brigedi na Vikosi ilifanya kazi na kutekeleza majukumu hayo kwa umahiri na ufanisi wa hali ya juu na hatimaye wakati ulifika na kuona ipo haja ya kuboresha muundo wa Jeshi letu ndipo Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ikazaliwa.

Wakati tunaadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tarehe 01 Septemba 2014, Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu tayari imetimiza miaka sita tangu kuanzishwa kwake mnamo tarehe 25 Disemba 2007 kabla ya kuzinduliwa rasmi tarehe 04 Machi 2009 na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu yapo katika Kijiji cha Msangani, Wilaya ya Kibaha katika Mkoa wa Pwani ambapo Mkuu wake wa Kwanza kuiongoza Kamandi alikuwa Luteni Jenerali Wynjones Kisamba(mstaafu), wakati huo akiwa Meja Jenerali.

Meja Jenerali Salim Mustafa Kijuu (mstaafu) aliteuliwa kuongoza Kamandi hiyo mnamo mwaka 2012, akiwa ni Kamanda wa Pili. Kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu kumerahisisha na kuimarisha kwa kiasi kikubwa utendaji kazi wa Jeshi kwa ujumla. Tangu ilipoanzishwa, Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu imeweza kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Makamanda waliotangulia. Kwasasa Kamandi hii inaongozwa na Meja Jenerali Sharif Othman akipokea kijiti hicho toka kwa Meja Jenerali James Mwakibolwa ambae kwa sasa ni Luteni Jenerali.

Majukumu ya Kamandi

Pamoja na majukumu makubwa yanayotekelezwa na Kamandi hii, pia zipo shule chini ya kamandi kama vile Shule ya Mafunzo ya Infantria (SMI) ambayo inatoa mafunzo bora kwa Jeshi la Nchi Kavu na kuwaandaa maafisa na askari wa JWTZ. Mafunzo ndio uti wa mgongo katika utendaji kijeshi kwasababu huwajengea maafisa na askari uwezo katika kutekeleza majukumu yao ya msingi, mafunzo yamepewa kipaumbele cha pekee katika Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu.

Pia Kamandi huendesha Shule za Mizinga (School of Artillery), Shule ya Mafunzo ya Vifaru (SMV) na Shule ya Uhandisi wa Medani.

Umuhimu na matumizi ya taaluma na mbinu zitolewazo na shule hizi huonekana kwa urahisi na wepesi pale Kamandi inapokuwa imepewa jukumu katika uwanja wa medani. Mafunzo yanayotolewa na shule hizo ni kwa ajili ya kuwaandaa maafisa na askari kwa kuwajengea uwezo wa kufanya kazi na kamandi nyingine wakati wa vita.

Ili Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu iweze kufanyakazi zake kwa ufanisi katika kurahisisha utendaji na utoaji huduma kwa kamandi nzima kuanzia Makao Makuu ya Kamandi hadi kwenye Vikosi na Shule. Matawi matano yameundwa na kukabidhiwa utekelezaji wa majukumu hayo, matawi hayo ni pamoja na Tawi la Utumishi, Tawi la Fedha, Tawi la Oparesheni na Mafunzo, Tawi la Usalama na Utambuzi pamoja na lile la Ununuzi na Ugavi.

Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, imekuwa na majukumu ya Kitaifa na Kimataifa kwa vile ina jukumu la kuandaa maafisa na askari wanaoshiriki katika ulinzi wa amani nchini Sudan, Congo (DRC) na Lebanon.

Kwa hapa Tanzania, majukumu ya msingi ya Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ni pamoja na kulinda na kuimarisha usalama wa mipaka ya nchi kwa kushirikiana na Kamandi ya Anga na Kamandi ya Wanamaji. Kamandi hii hushirikiana na Kamandi nyingine ili kuleta ufanisi na tija katika suala la utendaji kazi na kulifanya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liwe la kisasa zaidi.

Aidha wakati wa Amani, Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ina wajibu mkubwa wa kuzisaidia mamlaka za kiraia katika kukabiliana na maafa pindi yanapotokea bila kusahau kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa Ulinzi na Usalama wa nchi na mipaka yetu dhidi ya adui yeyote awe kutoka ndani au nje ya mipaka ya Tanzania.

Tangu kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, yapo mafanikio ya kujivunia licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Kamandi hiyo, miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kulinda mipaka ya taifa letu na kuendelea kudumisha amani na utulivu hapa nchini. Kamandi imeweza kukabiliana na maafa yanayojitokeza katika nchi yetu kwa ujasiri wa hali ya juu kama vile mafuriko yaliyotokea katika Mikoa ya Morogoro na Dodoma. Kamandi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuyakabili maafa hayo kwa kujenga daraja la muda katika kijiji cha Gulwe Wilayani Mpwapwa.

Katika kukabiliana na mafuriko hayo Dodoma Kamandi ilijenga makazi ya muda katika kambi nne tofauti ambazo ni Kambi ya Chanzuru, Mazulia na Mkoani Morogoro katika Wilaya ya Kilosa, mafuriko yaliyosababishwa na Mto Mkondoa na kuleta maafa kwa Vijiji vya Mkondoa na Kimamba na kutoa huduma za afya bure na maji safi kwa wakazi walioathirika na mafuriko hayo. Kamandi imeweza kujenga mahusiano mazuri kwa asasi mbalimbali za kiraia katika kuimarisha na kutunza suala la amani na ushirikiano katika taifa. Kwa ujumla, utendaji kazi wa Kamandi hii unaimarika siku hadi siku.