Kikao cha 40 cha Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kimehitimishwa rasmi tarehe 16 May, 2025 jijini Arusha, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujadili mambo mbalimbali ya kisera na mipango ya ushirikiano wa kijeshi baina ya nchi wanachama.
Kikao hicho kilichofanyika chini ya Uenyekiti wa Dkt.Patrick Mariru Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi wa Kenya ambaye alimwakilisha Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa kikao hicho Dkt. Patrick Mariru ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa mapokezi mazuri na ukarimu walioupata kutoka kwa Watanzania katika kipindi chote cha Kikao hicho.
Aidha, amezitaka nchi wanachama kupitia majeshi yake kuendeleza umoja, mshikamano na kuimarisha ushirikiano na mazoezi ya pamoja katika masuala ya Ulinzi ili kuifanya Jumuiya hiyo kuwa sehemu salama dhidi ya matishio ya kiusalama.
Viongozi mbalimbali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walihudhuria kwenye kikao hicho, akiwemo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Veronica Mueni Nduva. Kwa upande wa Tanzania, uliwakilishwa na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Luteni Jenerali Salum Othman kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stargomena Tax.
Jumla ya nchi wanachama idadi nane ambazo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Uganda na mwenyeji Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilishiriki.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.