KAMANDI YA JESHI LA WANAMAJI
Historia ya Kamandi
Kamandi ya Wanamaji ni kati ya Kamandi tatu zinazounda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Kamandi ilianza wakati wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Jeshi la kisasa lenye mtazamo wa kizalendo wa kuwalinda wananchi wake.
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji ilianzishwa rasmi mnamo tarehe 06 Disemba1971, baada ya nchi kuhitaji kuwa na ulinzi wa mipaka yake kwa upande wa bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Maeneo yote hayo ni mipaka ya Tanzania na nchi jirani zinazoizunguka Tanzania. Katika Bahari ya Hindi Tanzania inapakana na Comoro, Shelisheli na Madagascar. Katika Ziwa Victoria Tanzania inapakana na Kenya na Uganda, katika Ziwa Nyasa Tanzania inapakana na Malawi na Msumbiji na katika ziwa Tanganyika Tanzania inapakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi.
Jitihada na juhudi za ziada zilizofanywa na serikali na Makamanda wa Jeshi zilizaa matunda na kufanikiwa kuanzisha Kamandi ya Wanamaji. Jiwe la msingi la kuanza kujenga miundombinu ya Jeshi la Wanamaji liliwekwa na aliyekuwa Rais wa kwanza na Amiri Jeshi Mkuu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere tarehe 06 Disemba 1970 na kukamilika baada ya mwaka mmoja kwa msaada wa Jamhuri ya Watu wa China. Miundombinu iliyojengwa ni pamoja na majengo, karakana, sehemu za kuegesha meli na barabara.
Wanajeshi wa kwanza wa Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania walipata mafunzo yao ya Wanamaji nchini China na baada ya hapo wengine walipewa mafunzo kwa awamu ambapo wataalam wa Kichina wamekuwa wakija Tanzania na wakati mwingine Wanamaji wetu huenda mara kwa mara nchini China kwa ajili ya mafunzo na kubadilishana uzoefu. Kutokana na serikali ya Tanzania kuwa na sera nzuri ya mambo ya nje, Tanzania imekuwa na marafiki wengi wanaotoa nafasi kwa Kamandi kupeleka mabaharia wengine katika nchi zao ili kufanya mafunzo na kubadilishana uzoefu. Nchi hizo ni pamoja na India, Misri, Pakistani na Afrika Kusini.
Wakati Kamandi ya Jeshi la Wanamaji inaanzishwa, ilianza kama kikosi kilichokuwa kinaitwa NAVY FLOTTILA kikiwa na kombania za mapigano pamoja na Kiwanda, Utawala, Kikundi cha Umeme na ile ya Rada. Hii kombania ya Rada ilikuwa na viteule sehemu mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Tanzania visiwani. Makao Makuu ya Kamandi yaliwekwa kwa muda katika eneo la Wazo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Idadi ya meli zilizokuwepo wakati huo zilikuwa 13 ambapo Meli za kivita zilikuwa kumi na nyingine tatu zilikuwa za utawala. Meli za kivita zilikuwa katika makundi mawili, kundi la kwanza ni Gun Boats, lililokuwa na meli sita na kundi la pili ni Topido ambalo lilikuwa na Meli nne. Katika meli nyingine tatu ilikuwepo boti ya mawasiliano yaani ‘topido recovery boat na tag boat'.
Madhumuni ya Kuanzishwa Kamandi ya Wanamaji
Kuanzishwa kwa Kamandi ya Wanamaji ilikuwa ni jambo muhimu la kimkakati kwa ajili ya kuendelea kuhakikisha kuwa mipaka yote inakuwa salama.
a. Kukamilisha muundo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwa kila nchi yenye Bahari, Maziwa na Mito mikubwa inahitaji Kamandi ya wanamaji ili kusimamia ulinzi wa maeneo hayo.
b. Kuhakikisha mipaka yote katika Bahari, Maziwa na Mito mikubwa inakuwa salama wakati wote.
c. Kuwapa ulinzi wa kutosha Wananchi wanaoishi kwa kujishughulisha na uvuvi Baharini, Maziwa na mito mikubwa ili waweze kujipatia kipato chao na kuinua uchumi wa Tanzania.
Kuwa Kamandi Kamili
Ujenzi wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji uliendelea kwa malengo ya kupata Kamandi kamili inayoweza kujitegemea katika kudhibiti mipaka yote ya Bahari, Maziwa na Mito. Kadiri muda ulivyokuwa ukienda mabadiliko yalikuwa yakitokea katika kikosi hiki cha Wanamaji, hadi ilipofika mwaka 1983, Serikali ilikuwa imewekeza na kuhakikisha Kamandi ya Jeshi la Wanamaji nchini Tanzania imeanza kufanyakazi kama ilivyokusudiwa. Uanzishwaji wa Kamandi ya Wanamaji ulienda sambamba na kuzibadilisha Kombania kuwa vikosi chini ya Kamandi hiyo ili kuzipa mamlaka kamili ya kiutendaji kama Kamandi ya Wanamaji.
Kombania ya utawala ikaitwa kikosi cha utawala ambacho ndicho kikosi cha Makao Makuu ya Jeshi la Wanamaji kikiwa na kazi ya kuratibu shughuli zote za utawala zinazoihusu kamandi. Kombania ya Lojistiki nayo ikawa kikosi cha Utawala ambacho Majukumu yake makubwa ni shughuli zote zinazohusu ununuzi, usambazaji na usafirishaji wa mahitaji ya vifaa vya Kamandi ya Wanamaji.
Kamandi ya Wanamaji inayo Shule ya Kijeshi ya Ubaharia iliyoanzishwa mwaka 1979 ikiitwa Training Wing hadi mwaka 1980, ilipobadilishwa jina na kuitwa SKU. Shule hiyo ni sehemu ya juhudi za Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kujitegemea kwa kuwajengea uwezo watendaji wake.
Kamandi iliendelea kukua na mwaka 1991 iliongeza ujenzi wa majengo ya Shule kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa maafisa na askari ili kukidhi hitajio la mabaharia hapa nchini. Pia ujenzi wa mwaka 1991 ulienda sambamba na kuwa na vifaa vingi vya kisasa viliongezwa ili kukidhi haja ya sayansi na teknolojia ya kisasa. Shule ya mabaharia imekuwa injini ya Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, mafunzo ya ulinganifu hufanyika kwa ajili ya maafisa ambao hufanya kozi na mafunzo yao katika Kamandi ya Jeshi la Wanamaji na kutoka Kamandi nyingine ili kuleta ufanisi, mafunzo hayo ni muhimu kwa maafisa na askari wanaomaliza mafunzo ya awali kutoka vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Huduma za Kijamii
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sera ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kuweka maslahi ya wananchi mbele. Kamandi imekuwa ikitoa huduma ya afya bure kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya kambi.
Pamoja na huduma za afya kuna huduma ya elimu inayotolewa na Kamandi kwa vijana wanaoishi jirani na shule ya sekondari Kigamboni. Wanafunzi wengine wanatoka mbali kwenda kusoma pale na wamekuwa wakifaulu vizuri na kuchaguliwa kujiunga na masomo ya elimu ya juu.
Huduma zote hizo za kijamii zinatolewa kwa wanajeshi na familia zao, watumishi wa umma na jamii inayoizunguka Kamandi. Madhumuni ya kuanzishwa kwa shule ya sekondari Kigamboni ilikuwa ni kwa ajili ya Wanajeshi wenyewe ambao walihitaji kujiendeleza kielemu lakini pia na kuwasomesha watoto wao, ikiwa ni pamoja na watumishi wa umma na hata watoto wa jamii inayoizunguka kamandi.
Kamandi ya Wanamaji imewahi kuongozwa na makamanda mbalimbali kwa nyakati tofauti kwa mafanikio makubwa.
Meja Jenerali (mstaafu) Rowland L Makunda aliteuliwa kuongoza Kamandi kuanzia mwaka 1971 hadi 1983. Meja Jenerali (mstaafu) Rowland L Makunda alikuwa na historia ndefu katika Kamandi ya Wanamaji, alianza kuongoza Kamandi wakati bado ilikuwa ni kikosi tu cha wanamaji.
Meja Jenerali Rowland Makunda ana historia ya kipekee ambapo ndiye aliyekuwa kiongozi wa maonesho ya kikundi cha utimamu wa mwili (Fitness Training Display) siku Tanganyika inapata uhuru kutoka kwa mkoloni na vilevile alishiriki kikamilifu katika vita ya Kagera.
Meja Jenerali (mstaafu) Ligate Sande aliteuliwa kuongoza Kamandi kuanzia mwaka 1983 hadi 2002 alipostaafu utumishi Jeshini.
Brigedia Jenerali (mstaafu) Joachim Lisakafu aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuanzia mwaka 2002 hadi 2006 alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri.
Meja Jenerali (mstaafu) Said Omar aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuanzia mwaka 2006 hadi 2013 alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri.
Brigedia Jenerali Rogastian Lasway aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la wanamaji kuanzia mwaka 2013. Alipandishwa cheo na kuwa Meja Jenerali na kuteuliwa tena kuendelea kuongoza Kamandi hiyo hadi 2016.
Rear Admiral Richard Makanzo aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuanzia Aug 2016 hadi Aug 2021.
Rear Admiral Michael Mumanga aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuanzia Aug 2021 hadi Feb 2022.
Rear Admiral Ramson Mwaisaka aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuanzia Feb 2022 hadi Okt 2023.
Rear Admiral Ameir Hassan aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuanzia Okt 2023 hadi sasa.
Wajibu Mwingine wa Kamandi ya Wanamaji kwa Karne hii.
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji imetoa mchango mkubwa katika jitihada za kimataifa za kupambana na uharamia katika bahari ya Hindi. Miaka ya hivi karibuni Dunia imekumbana na changamoto za uharamia katika bahari ya Hindi. Sehemu kubwa ya changamoto hizo za uharamia baharini zimetokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini Somalia. Kwa hiyo wapiganaji wanatafuta njia za kupata pesa ili kuendelea na vita hiyo. Njia mojawapo wanayotumia ni pamoja na kuendesha uharamia wa kuteka Meli zote zinazopita katika Pwani ya Afrika Mashariki.
Wanamaji wa Tanzania wanasaidia jitihada za kuzuia uharamia katika Pwani ya Tanzania na Pwani ya Afrika Mashariki. Jitihada hizo za Wanamaji zina lengo la kulinda Meli za kibiashara, pamoja na shughuli nyingi za kiuchumi zinazofanyika katika Bahari ya Hindi kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa za biashara husafirishwa kwa njia ya bahari.
Aidha, uharamia ukiachwa uendelee utaathiri usafiri wa njia ya Bahari ya Hindi na nchi zitakazoathirika na uharamia ni pamoja na nchi zote zinazotumia bandari ya Dar es Salaam za Zambia, Rwanda, Malawi, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hivyo uharamia una madhara makubwa kwa maendeleo ya kiuchumi kwa ukanda huu na dunia kwa ujumla.
Jeshi la Wanamaji wa Tanzania limekuwa likifanya doria inayotoa mchango mkubwa katika jitihada za kikanda na za ulimwengu katika kutokomeza uharamia baharini. Msako wa maharamia umekuwa na mafanikio makubwa kwa vile Wanamaji wamekuwa wakishirikiana na majeshi ya nchi rafiki kama Jeshi la Wanamaji wa Afrika Kusini katika kuendesha msako huo.
Itakumbukwa kuwa ilipofika mwishoni mwa mwaka 2003, vyombo vingi vya baharini vilianza kuripoti kuhusu maharamia wa kisomali waliokuwa wakiteka Meli nyingi katika ukanda wa Ghuba ya Aden na maeneo mengine ya bahari ya Hindi. Baada ya Meli kuanza kupita Bahari Kuu, maharamia nao walisogeza mitego yao katika pwani ya Afrika Mashariki na kwa Tanzania mwaka 2010 matukio 18 yaliripotiwa katika kipindi cha miezi kumi (10).
Mwaka huohuo, iliripotiwa kwamba maharamia wamekuwa wakiendeleza uharamia huo umbali wa kilometa 1,850 katika bahari ya Hindi ili kukwepa doria zinazofanywa na vikosi vya wanamaji katika maeneo yao ya utekaji ya awali. Maharamia wamekuwa wakiteka meli jirani zaidi na India kuliko Pwani ya Afrika kwa vile Meli zilikuwa zinapita Bahari Kuu ili kukwepa mitego ya maharamia hao.
Tishio la maharamia wa kisomali katika pwani ya Tanzania kwa meli zinazoelekea bandari ya Dar es Salaam yalihusu makundi ya vijana wanaokadiriwa kuwa 1,500 ambao walikuwa wakizunguka katika pwani ya Afrika Mashariki kwa malengo ya kuteka Meli za biashara. Wengi wa vijana hao wa kisomali walibainika kuwa na umri kati ya miaka 20 na 35 baada ya kukamatwa na kuhojiwa, waligundua kuwa wengi wa vijana hao walikuwa wavuvi hivyo wana ufahamu wa bahari na huutumia ufahamu huo kuzisaka meli baharini. Wanamgambo na wapiganaji wa vita nchini Somalia nao hushiriki kikamilifu katika kuteka Meli kwa vile wana silaha za kisasa zinazowawezesha kutekeleza uhalifu huo.
Aidha, kuna hali inayoonesha kwamba kuna ushiriki wa watalaamu wa simu za satellite, global position system (GPS) na matumizi ya teknolojia nyingine zenye uwezo mkubwa wa kujua mwelekeo na mahali ilipo meli, ushirikiano huo wa maharamia hukamilisha muundo wa vikosi kamili vya utekaji meli baharini.
Uharamia katika bahari ya Hindi, pwani ya Tanzania umekuwa ukitumia mbinu zinazotumiwa katika maeneo mengine katika bahari ya Hindi ambapo boti ziendazo kasi hubeba maharamia watatu hadi saba na kawaida huziteka meli kwa kutumia silaha nyepesi na ndogo, silaha nzito kama bunduki za rashasha (Machine guns), na wakati mwingine hubeba hata roketi na silaha za kupambana na vifaru (RPG). Meli zinazotekwa hupelekwa eneo la Pwani ya Somalia ambapo huhitaji fedha taslimu za kugomboa meli hizo zikiwa na mateka katika eneo zinaposhikiliwa.
Mazungumzo ya kuzigomboa hizo meli hufanyika nje ya Somalia kwa kuwashirikisha watu wenye mawasiliano na watekaji wa meli. Pamoja na kuteka meli hizo, maharamia huwatumia mabaharia na wafanyakazi wengine wa meli zilizotekwa kama ngao pindi wanaposhambuliwa na meli za kivita au waokoaji wa Kimataifa na hivyo hufanya kazi ya uokoaji kuwa ngumu.
Kutokana na juhudi za kimataifa katika kukabiliana na uharamia kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, maharamia wamebadili mbinu na aina ya meli wanazoziteka, awali walikuwa wakiziteka meli za uvuvi au meli ndogo za mizigo, siku hizi hulenga meli za kemikali, boti kubwa za uvuvi, meli kubwa za mizigo na hata meli za kifahari za kitalii.
Meli ya mizigo ya MV Asphalt venture iliyokuwa ikisafiri kutoka Kenya kwenda Afrika Kusini mnamo Septemba 2010 ilitekwa umbali wa kilometa 180 kusini mashariki mwa jiji la Dar es salaam. Baada ya kutekwa meli hiyo ilibadili mwelekeo ghafla kutoka ule wa awali kuelekea Durban na kuanza kuelekea pwani ya Somalia, pia meli hiyo ilikuwa haijibu miito ya radio za mawasiliano. Baada ya kuwa mateka kwa miezi kadhaa wafanyakazi wachache kati ya 15 wa meli hiyo waliachiwa huru baadhi waliendelea kushikiliwa. Katika hali isiyo ya kawaida maharamia walikuwa na madai ya ziada, ingawa fedha za kugombolea mateka zililipwa, maharamia hao waliendelea kudai kuachiwa huru kwa maharamia 100 wa Kisomali waliokamatwa na Serikali ya India.
Maharamia hutumia Meli za uvuvi wanazoziteka kama meli mama kwa ajili ya kuwezesha uharamia sehemu mbalimbali ambapo ni mbali na Pwani ya Somalia kwa mfano, Pwani ya Dar es Salaam na maeneo mengine mbali na Pwani ya Somalia. Meli hizi zina urefu wa mita 30 na zinaweza kuchukua watu zaidi ya ishirini (20), Jahazi moja liliwahi kukamatwa na kamandi ya Jeshi la Wanamaji wa Tanzania mnamo mwaka 2010 likiwa na maharamia 10 na wafanyakazi saba (7). Boti ya mwendo kasi inayotumika kwa ajili ya utekaji nyara inaweza kuhifadhiwa na kufichwa katika meli kubwa na kutumika wakati wa uvamizi wakati wa utekaji meli. Meli hizi pia zina uwezo wa kuhifadhi vifaa na chakula, hivyo kuwawezesha maharamia kuishi muda mrefu Baharini.
Pia Jeshi la Wanamaji wa Tanzania limekuwa likikabiliana na tishio la kutaka kutekwa kwa vituo na vifaa vya utafiti wa mafuta na gesi na maharamia katika Pwani ya Bahari ya Hindi.
Kwa sasa maharamia wamepanua maeneo ya utekaji wa Meli wakilenga meli za utafiti na uchimbaji wa mafuta unaofanywa katika bahari ya Hindi kusini mwa Tanzania eneo la Mtwara. Mashambulizi dhidi ya meli za utafiti mwaka 2010 yanabainisha kwamba maharamia walilenga kuwateka wataalamu wanaofanya kazi ya utafiti wa mafuta katika miamba ya bahari.
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji imeendelea kuendesha doria za mara kwa mara na kuwawezesha wawekezaji kuwa na imani na usalama wao. Bila hatua madhubuti za kupambana na uharamia huo ingepelekea kukwama kwa mipango mizuri ya serikali katika kuhakikisha kuwa utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi unafanyika katika mazingira salama.
Wawekezaji wamekuwa na jukumu la kuwalipa walinzi katika eneo lao la utafiti dhidi ya maharamia. Kimsingi athari za uharamia zimekuwa kubwa na zimeathiri sekta mbalimbali. Maharamia katika ulimwengu huu wamekuwa wakilipwa mamilioni ya dola za kimarekani na makampuni ya meli zinazotekwa.
Aidha, kutokana na uharamia baharini malipo ya bima kwa usafirishaji wa bidhaa kupitia bandarini zimeongezeka. Meli zimekuwa zikilazimika kuzunguka umbali mrefu ili kukwepa maeneo yanayofahamika kuwa na maharamia. Mzunguko kupitia Afrika Kusini katika rasi ya Tumaini Jema, umekuwa ukichelewesha mizigo inayohitajika kwa haraka na nchi zinazotegemea bandari ya Dar es salaam.
Kutokana na hali ilivyo, maharamia wanavuruga mfumo wa biashara ya usafirishaji baharini ambayo inategemewa katika uchumi wa dunia kwa asilimia kubwa na matokeo yake ni kushuka kwa uchumi au pato linalotokana na biashara hizo. Ongezeko la gharama za usafirishaji hugharimiwa na mteja wa usafiri huo na hivyo kuchangia ongezeko la bei ya bidhaa kwa watumiaji wa bidhaa hizo.
Ongezeko la gharama za usafirishaji mizigo hususani yenye rasilimali kama mafuta, huduma za ukuaji wa uchumi kutokana na ukweli kuwa bidhaa hiyo ndiyo kichocheo pekee cha maendeleo ya uchumi popote duniani. Misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Somalia walio katika mateso ya vita ya muda mrefu ipo mashakani na wakati mwingine hulazimika kupitia nchi jirani ili kuwafikia wahanga wa vita hiyo. Kuna uwezekano mkubwa kuwa siku moja meli ya mafuta inaweza kushambuliwa na kusababisha madhara makubwa kwa mazingira, viumbe wa baharini na ukanda mzima wa pwani ya Afrika Mashariki kuchafuka.
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji wa Tanzania linashiriki katika jitihada za kidiplomasia, kimahakama na kisheria ili kuhakikisha kuwa kuna utatuzi wa tatizo la uharamia katika Pwani ya Afrika Mashariki na duniani kote. Tanzania inaendelea kuunga mkono jitihada za Kimataifa za uundwaji wa Serikali yenye mamlaka nchini Somalia na aliyekuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika nchi ya Somalia ni Mwanadiplomasia Mtanzania Ndugu Augastin Mahiga ambaye amemaliza muda wake hivi karibuni.
Lengo ni kupata Serikali itakayosimamia usalama wa pwani na bahari dhidi ya uharamia na kuwasaidia vijana wa kisomali kupata ajira na kuwa na vyanzo halali vya mapato. Ushiriki wa Tanzania katika ulinzi wa bahari na hasa katika ngazi ya kanda umezidi kuimarika kwa vile nchi jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki na nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) zinashirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha ukanda huu unakuwa salama wakati wote.
Meli za kivita za Kamandi ya Jeshi la Wanamaji zina mfumo wa kisasa wa mawasiliano. Teknolojia hiyo ya mawasiliano inarahisisha mawasiliano kati ya meli moja na nyingine kuwa ya uhakika. Kamandi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwafukuza maharamia mbali na pwani ya Tanzania na wakati huo huo nyendo za maharamia zimekuwa zikifuatiliwa na Jeshi la Wanamaji kutoka Jumuiya ya Ulaya. Jitihada za kupambana na uharamia katika Kamandi ya Wanamaji zinawashirikisha Polisi wa Tanzania, hiyo yote imetokana na kutungwa kwa sheria kali dhidi ya maharamia. Meli za vikosi hivyo zinaweza kuwakamata na kuwafungulia mashtaka maharamia bila kujali walikamatwa wapi.
Sheria ya uharamia inatoa ujumbe kwa watu wote wanaojihusisha na uharamia kukamatwa na kushitakiwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa dhidi ya uharamia. Kamandi ya Wanamaji wa Tanzania walipambana na maharamia baharini kwa siku nzima mnamo Septemba 2010 ambapo boti ya Wanamaji ilishambuliwa wakati ilipokuwa inapambana na maharamia 50 waliokuwa na silaha. Wanamaji wawili (2) wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walijeruhiwa katika pambano hilo, Wanamaji wa Jeshi wakishirikiana na Polisi walifanikiwa kumkamata haramia mmoja. Katika tukio lingine mwezi huohuo, Wanamaji wa Tanzania walikuwa katika meli ya utafiti wa mafuta walifanikiwa kuwashambulia maharamia waliokuwa wakijaribu kuteka meli hiyo.
Operesheni za baharini zimekuwa zikiungwa mkono na ushirikiano wa Kimataifa katika doria na ukusanyaji taarifa za Kiintelijensia. Meli za mizigo zimekuwa zikihimizwa kuzingatia mbinu bora za usimamizi na uendeshaji wa biashara zao. Meli za Kijeshi za Tanzania na Wanamaji wa nchi za Jumuiya ya Ulaya zilipewa tahadhari kuhusu hali ya Meli ya MV Mississippi Star mnamo Septemba 2010 baada ya kushambuliwa na maharamia Kaskazini Mashariki mwa Jiji la Dar es salaam. Maharamia walikuwa wakitumia bunduki za rashasha na mabomu ya kutupa kwa mkono, maharamia walishindwa kuiteka meli hiyo ya mafuta baada ya nahodha wa meli kuongeza mwendo kasi na kuwapiga chenga kuepuka mashambulizi.
Usalama wa bahari ya Hindi katika pwani ya Tanzania unaimarika siku hadi siku kwa kuongeza uwezo wa Wanamaji wa JWTZ katika kupambana na uharamia. Pia JWTZ linashirikiana na Makampuni yanayofanya utafiti wa mafuta na gesi ili kulinda sekta hii muhimu ya uchumi nchini. Aidha, JWTZ limeanzisha ushirikiano wa karibu na kampuni za usafirishaji baharini na mawakala wa meli ili kuweza kupambana kikamilifu na maharamia. Meja Jenerali Omar Said (sasa mstaafu) aliyekuwa Mkuu wa Kamandi ya Wanamaji alibainisha kwamba ukanda wa pwani ya Tanzania wenye kilometa 800 unapaswa kuwekwa kwenye kampeni maalumu ya kupambana na uharamia. Taarifa za kiintelijensia zinabainisha kwamba maharamia wa Kisomali wanaweza kuweka kambi katika fukwe zinazofikika kirahisi.
Kambi moja ya maharamia iliyotelekezwa iligunduliwa na wanamaji wa Tanzania mwaka 2010 Mkoani Lindi, Kusini Mashariki mwa Tanzania. Lakini pia msako unaendelea ili kubaini kambi nyingine popote zilipo katika ukanda wa Pwani yetu. Tanzania kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama inafanya kazi hiyo kuwa endelevu, Kamandi ya wanamaji inaendelea kushirikiana na jumuiya ya Kimataifa katika nyanja za kiintelijensia na kuhakikisha usalama wa vyombo vinavyotumika majini na hasa baharini unakuwepo wakati wote.
Mafanikio ya Wanamaji
Tangu kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuna mambo mengi ya kujivunia ambayo yamefanywa na kamandi hii kwa ajili ya taifa letu;
a. Ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi pande zote za bahari ya Hindi na bandari zote nchini umeimarika. Hii imeifanya nchi yetu kutoingiliwa na adui kirahisi na imekuwa na mipaka ya bahari iliyo salama.
b. Kamandi iliweza kushiriki kikamilifu katika vita ya Kagera ambapo ilitoa mchango mkubwa kupitia kwenye ziwa Victoria. Meli vita aina ya Topido Squadron chini ya Meja Joachim Lisakafu walifanikiwa kuangusha ndege mbili za adui zilizokuwa zikivuka ziwa Victoria kuja kushambulia nchini. Baadaye alipandishwa cheo hadi kufikia cheo cha Brigedia Jenerali na kuwa Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji hadi alipostaafu na cheo hicho.
c. Kamandi inashirikiana na Wizara ya Ujenzi katika kutengeneza vivuko mara tu vinapoharibika, na kutoa elimu ya usalama baharini kwa wananchi.
d. Kamandi inashirikiana na wizara ya uvuvi na mifugo katika kupambana na wavuvi haramu katika eneo lote la bahari na maziwa.
e. Kamandi imefanikiwa kupambana na kuzuia uhalifu na uharamia baharini kwa kushirikiana na Majeshi rafiki ya Marekani, Uingereza, China pamoja na Afrika ya Kusini.
f. Mahusiano yetu kimataifa yameongezeka, hii ni kutokana na Jeshi letu la Wanamaji kushiriki kutoa mihadhara katika makongamano ya kimataifa yahusuyo mambo ya Jeshi la wanamaji. Mfano katika mikutano ya Jumuiya za Kikanda kama vile Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
g. Kamandi ya Jeshi la Wanamaji ilishiriki vilivyo katika operesheni ya kumuondoa Kanali Bakari huko Comoro aliyeasi na kujitangazia madaraka ya kuiongoza nchi hiyo.
h. Kamandi inashiriki katika operesheni mbalimbali za uokoaji mara tu ajali inapotokea, mfano ilipotokea kuzama kwa meli ya MV Bukoba mwaka 1996 huko Mwanza, kamandi hii kwa kushirikiana na wapiga mbizi kutoka nchi ya Afrika Kusini ilifanya uokoaji wakati wa ajali hiyo.
Matarajio ya Kamandi
Kamandi ya Wanamaji kama ilivyo kwa Kamandi nyinginezo, inayo malengo iliyojiwekea kwa ajili ya kutimiza wajibu na majukumu yake kama:-
a. Kuendelea kuimarisha ulinzi wa mipaka yote ya bahari na maziwa ili kuendelea kuifanya Tanzania kuwa salama wakati wote.
b. Itaendelea kushirikiana na majeshi rafiki kuhakikisha kuwa Bahari ya Hindi katika Pwani ya Afrika Mashariki inaendelea kuwa salama.
c. Kamandi itaendelea kutoa mafunzo kwa watendaji wake mara kwa mara iii kwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia mpya.
d. Kamandi itaendelea kushiriki mazoezi ya ndani na yale ya kimataifa kwa ajili ya kubadilishana uzoefu
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.