KAMANDI YA JESHI LA ANGA
Historia ya Kamandi ya Jeshi la Anga.
Kamandi ya Jeshi la Anga ni moja ya Kamandi muhimu zinazounda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kiutendaji, kivita na kiutawala. Kamandi ya Jeshi la Anga inayo majukumu ya ziada ya msingi katika kutimiza wajibu wake wa ulinzi wa Anga la Tanzania. Kamandi hiyo inao uzoefu wa kusafirisha maafisa na askari wakati wa amani na dharura, pia husaidia mamlaka za kiraia katika kutimiza wajibu wake na kusafirisha mizigo. Juhudi za awali za kuunda nguvu za Jeshi la Anga ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania zilianza mapema mwaka 1964 pale ambapo kikundi cha maafisa kadhaa walipelekwa nchini Israeli na Ujerumani ya Magharibi wakati huo kusomea urubani. Hata hivyo, wanafunzi waliokwenda kujifunza urubani katika nchi ya Ujerumani ya Magharibi hawakuweza kumaliza mafunzo ya urubani kutokana na kuvunjika kwa uhusiano wa kibalozi baina ya Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi mwaka 1965.
Baada ya jitihada za muda, hatimae kikosi cha usafirishaji wa anga kilianza operesheni mwaka 1969 kikiwa na ndege mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ndege nne aina ya OTTER na zilizosalia za CARRIBOU. Wakati wote wa chimbuko la nguvu za anga shughuli zote za kioperesheni zilizohusu vikosi na vitengo vya ulinzi wa anga viliongozwa na Tawi la Operesheni na Mafunzo (COT) la Makao Makuu ya Jeshi.
Mwaka 1971 kilianzishwa kikosi maalum cha mizinga ya kutungulia ndege kikiongozwa na Kapteni Abdallah, makao yake yakiwepo Mgulani. Maafisa wa mwanzo walipelekwa Pakistan na India kwa mafunzo ya mizinga hiyo. Mwaka huohuo Rais na Amiri Jeshi Mkuu (mstaafu) Mwl. Julius K. Nyerere aliagiza Jeshi lipatiwe ndegevita. Mwaka 1973 timu ya marubani wanafunzi 48 wakiongozwa na Meja JE Luhanga(alistaafu akiwa Meja Jenerali) walihitimu mafunzo yao nchini China na wakaanzisha kikosi cha kwanza cha ndegevita
Maendeleo makubwa yalifanyika katika kipindi cha miaka mitano ambapo idadi ya vikosi na zana za Ulinzi wa Anga viliongezeka. Mwaka 1975 vikosi vya Rada vilianzishwa na kugawiwa kanda za uchunguzi wa Anga, kipindi hichohicho vikosi vya makombora matiifu ya kutungulia ndege (SAM) vilianzishwa katika miji mbalimbali.
Utaratibu wa utendaji kivita na mafunzo wa vikosi vyote vya ulinzi wa anga toka 1974 hadi 1982 ulifanywa na Tawi la Makao Makuu ya Jeshi (MMJ) la Chief of Air Defence (CAD) chini ya Kanali SA Hemedi, ambaye baadae alipandishwa cheo kuwa Brigedia Jenerali.
Majukumu ya Kamandi ya Anga.
a. Kutoa ulinzi wa Anga kwa maeneo muhimu ya kitaifa, kisiasa, kiuchumi na kwa Wananchi,
b. Kutoa ulinzi wa Anga kwa maeneo na vituo muhimu vya kijeshi na mkusanyiko wa Majeshi,
c. Kutoa msaada wa kimapigano kwa operesheni za Majeshi ya Nchi Kavu na Wanamaji,
d. Kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia hasa nyakati za maafa ya kitaifa na kusindikiza ndege za viongozi pia hukusanya taarifa za kiusalama,
e. Kuendeleza juhudi za mahusiano ya kijeshi na nchi nyingine kwa njia ya mazoezi ya pamoja.
f. Kushiriki katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.
Makamanda Waliowahi Kuongoza
Kamandi ya Jeshi la Anga, tangu ilipoanzishwa hadi hivi sasa imeongozwa na Makamanda saba wakiwamo wa vyeo mbalimbali ambapo cheo cha chini ni Kanali na cheo cha juu ni Meja Jenerali. Makamanda hao ni pamoja na Brigedia Jenerali Robert Mboma aliyeteuliwa kuongoza Kamandi kuanzia tarehe 15 Februari 1982 hadi tarehe 28 Machi 1985, na baada ya kupandishwa cheo kuwa Meja Jenerali Robert Mboma aliendelea kuongoza kuanzia tarehe 28 Machi 1985 hadi tarehe 28 Machi 1994 alipopandishwa cheo kuwa Jenerali na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi hadi alipostaafu utumishi kwa umri mwaka 2001. Kanali Geofrey Dahal aliteuliwa kuwa Kamanda wa Kamandi ya Jeshi la Anga tarehe 01 Julai 2003 hadi 28 Disemba 2003. Kanali Geofrey Dahal alipandishwa cheo kipya kuwa Brigedia Jenerali tarehe 28 Disemba 2003 na kuteuliwa kuendelea kuongoza Kamandi ya Jeshi la Anga hadi tarehe 25 Aprili 2005 alipofariki kwa ugonjwa. Brigedia Jenerali Charles Makakala aliteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga tarehe 02 Julai 2005 hadi tarehe 16 Octoba 2007 ambapo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Tawi la Mipango Makao Makuu ya Jeshi. Brigedia Festo Ulomi aliteuliwa kuwa Kamanda wa wanaanga kuanzia tarehe 17 Octoba 2007 hadi tarehe 11 Agosti 2009 baada ya kupandishwa cheo kipya kuwa Meja Jenerali aliteuliwa kuendelea kuongoza Kamandi ya Jeshi la Anga tarehe 12 Agosti 2009 hadi tarehe 19 Machi 2012 alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri. Brigedia Jenerali Joseph Kapwani aliteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga kuanzia tarehe 20 Machi 2012 hadi 16 Septemba 2012 alipopandishwa cheo kipya kuwa Meja Jenerali na kuteuliwa kuendelea kuongoza Kamandi hiyo hadi tarehe 31 Jan 2016 alipostaafu Jeshini kwa umri. Brigedia Jenerali George Ingram aliteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga kuanzia tarehe 01 Feb 2016 hadi alipopandishwa cheo kipya kuwa Meja Jenerali tarehe 03 Dec 2016 na kuendelea kuongoza Kamandi hiyo hadi tarehe 22 Aug 21 alipostaafu Jeshini kwa umri. Meja Jenerali Shabani Mani aliteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga kuanzia tarehe 23 Aug 2021 hadi sasa..
Ushiriki wa Kamandi Wakati wa Amani.
Tangu kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Anga, imetimiza wajibu wake kama ilivyokusudiwa kusaidia Taifa. Kamandi ya Jeshi la Anga imeshiriki kwa ukamilifu katika kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii pale inapohitajika kufanya hivyo kupitia kikosi chake cha usafirishaji. Kamandi ilishiriki kubeba chakula cha msaada (mahindi) kutoka Iringa na kusambaza katika mikoa mbalimbali wakati wa janga la njaa mwaka 1974.
Kamandi imesaidia katika uokoaji wa wahanga wa mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini kama vile Rufiji mwaka 1984 na 1997, Kilimanjaro na Tanga mwaka 1994, Tabora mwaka 1993, Mbeya na Shinyanga mwaka 2007 na Kilosa mwaka 2010.
Kutokana na uzoefu mkubwa Kamandi ya Jeshi la Wanaanga imekuwa ikishiriki kikamilifu katika mazoezi ya kikanda yanayolenga kuimarisha uwezo wa Jeshi katika kufanya uokoaji wakati wa majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi. Mazoezi ya kikanda ambayo Kamandi ya Jeshi la Anga imekuwa ikishiriki ni pamoja na mazoezi yanayoendeshwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Tanzania imekuwa ikishirikiana na Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Zambia, Malawi, Namibia, Angola na Swaziland pamoja na nchi mbalimbali duniani.
Kamandi ya Jeshi la Anga imeshiriki katika harakati za uokoaji (search and rescue) mfano katika kuopoa miili iliyotokana na ajali ya ndege ya Yemen visiwani Comoro ambayo ilisukumwa na mawimbi hadi kisiwa cha Mafia, ndege na helikopta za Kamandi zilitumika kwenye operesheni hiyo mwaka 2009 kwa mafanikio.
Mara kwa mara Kamandi ya Jeshi la Anga imekuwa mstari wa mbele kusaidia pale inapotakiwa kufanya hivyo. Mwaka 2011, ndege za Kamandi zilitumika kusafirisha vifaa vya msaada kwa wananchi wa Visiwa vya Zanzibar baada ya kutokea maafa ya meli ya abiria ya MV Spider Islander. Pia kamandi ilitumika kusafirisha vifaa kutoka Dar es Salaam kwenda uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kuwaokoa wachimba madini wakati wa ajali ya migodi kujaa maji na kuua wachimbaji madini huko Mererani mwaka 2008.
Mikakati ya Kamandi ya Jeshi la Anga ni kuendelea kuwa hazina ya Taifa katika kufunza marubani wapya, mafundi ndege, na kuwa na mtandao mpana wa kumiliki anga la Tanzania. Upo uzoefu wenye sura mbili; upande mmoja ni kutambua ujuzi na uzoefu wa mafundi na wahandisi wa Kamandi. Kamandi itaendelea kuwa hazina ya uongozi na kuendelea kudumisha nidhamu ya kazi iliyokwisha kuwekwa na Makamanda na wapiganaji waliowahi kufanyakazi katika Kamandi ya Jeshi la Anga kwa miaka mingi ijayo.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.