Posted On: Friday, 24th October 2025
Kikundi cha Polisi Jeshi cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kinachohudumu kwenye Ulinzi wa Amani nchini Lebanon chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UNIFIL) leo tarehe 24 Oktoba, 2025 kimejumuika na Mataifa mengine yanayoshiriki katika Ulinzi wa Amani nchini humo katika kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa (UN DAY) .
Maadhimisho hayo yamefanyika kwa gwaride maalumu lililoandaliwa na vikundi kutoka mataifa yanayoshiriki kwenye jukumu la Ulinzi wa Amani nchini humo.
Siku ya Umoja wa Mataifa huadhimishwa kila ifikapo tarehe 24 Oktoba ikiwa ni kumbukizi ya kuanzishwa kwa Umoja huo ambao ulianzishwa rasmi mwaka 1945.
Leo hii vikundi hivyo vinapoadhimisha Siku hiyo, Umoja huo unatimiza miaka 80 toka kuundwa kwake.
Vikundi vyetu vya Polisi Jeshi vimekuwa vikiliwakilisha vema Jeshi letu kwa kutekeleza majukumu yake kwa nidhamu, utiifu, uhodari, uaminifu na weledi wa hali ya juu na hivyo kuendelea kuliletea sifa nzuri Jeshi letu na Taifa kwa ujumla katika anga za Kimataifa.
Kutokana na sifa nzuri ambazo Jeshi limekuwa likijizolea kutokana na utekelezaji wake wa majukumu, Tanzania imeendelea kuaminiwa na kushiriki katika majukumu ya Ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali ikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Msumbiji.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.