HISTORIA YA JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA
Historia ya kazi na shughuli za ulinzi na usalama hapa Tanzania zilianza tangu zama za mababu zetu. Jamii nyingi zilizoishi katika maeneo mbalimbali hapa nchini zilikuwa na ulinzi wa jadi uliohusisha kila mwanajamii. Ulinzi wa jadi ulikuwa ndiyo msingi wa usalama wa jamii zote kwa wakati ule. Silaha zilizotumika na mababu zetu zilikuwa duni kama vile upinde, mikuki, mundu,mapanga na sime kama silaha za msingi kulinda jamii zao. Kila kabila lilikuwa na namna ya kuwaandaa vijana wao kujifunza matumizi ya silaha na baadaye vijana walipewa jukumu la kulinda jamii zao.
Bara la Afrika lilipata mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii baada ya Mapinduzi ya viwanda yaliyotokea huko Ulaya katika karne ya 19. Mkutano mkuu wa Berlin uliofanyika kuanzia mwaka 1884 hadi 1885 ulifuatiwa na mabadiliko makubwa ya nchi za kiafrika kutawaliwa kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Huu ndiyo mwanzo wa nchi nyingi barani Afrika kuanza kuwa chini ya majeshi ya kigeni.
Ujerumani ilijipatia uhalali wa kuitawala Tanganyika baada ya mkutano wa Berlin ulioligawa bara la Afrika katika vipande vya nchi bila ridhaa ya waafrika wenyewe. Jeshi la Kijerumani lilianzisha harakati za kufuta tawala za makabila mbalimbali hapa nchini ili kuwa na utawala mmoja na jeshi moja la kikoloni. Harakati hizo za Wajerumani zilipelekea baadhi ya makabila kupambana na Jeshi la Kijerumani, kwa vile utawala wa kijerumani ulilenga kuharibu mfumo mzima wa ulinzi wa jadi, siasa na uchumi wa wenyeji.
Vita ya Chifu Mkwawa mwaka 1890 ni mfano kamili unaoonesha kuwa baadhi ya makabila hapa nchini yalikuwa na ulinzi imara japokuwa yalikuwa yanatumia silaha duni. Hata hivyo, miaka michache baada ya Chifu Mkwawa kushindwa vita na Wajerumani, kulianza vita vya majimaji iliyopiganwa kuanzia mwaka 1905 hadi 1907.
Vita hiyo iliiweka historia ya Tanganyika katika ramani ya dunia kwa kuwa makabila mbalimbali yalitumia silaha zao za jadi kupinga uvamizi wa majeshi ya kigeni, lakini kwa umoja wao walisimama kidete kupambana Uafrika wao.
Kipindi hicho cha kuligawa Bara la Afrika kilileta mabadiliko ya kiulinzi na kiusalama kwa vile Waafrika walinyang’anywa haki yao ya kujilinda na ndiyo ukawa mwanzo wa majeshi ya kisasa kuanza kutumika hapa nchini.
Harakati za kijeshi hapa nchini ziliingia katika sura mpya baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kuanzia mwaka 1914 hadi 1918, Wajerumani walipoteza na kunyang’anywa makoloni waliyokuwa wanayatawala kama sharti mojawapo la kushindwa vita. Tanganyika iliwekwa chini ya uangalizi wa Uingereza na kwa udhamini wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kuanzia kipindi hicho muundo wa Jeshi rasmi lililoongoza Tanganyika lilijulikana kama Kings African Rifles (KAR).
Licha ya KAR kuwa Jeshi la Tanganyika iliyokuwa chini ya Uingereza, bado mfumo wa uandikishaji na ajira Jeshini haukuwa rasmi. Vijana walishirikishwa katika kazi za ulinzi pale walipohitajika. Wakati wa amani vijana walikuwa wakishiriki katika kazi za uzalishaji mali pamoja na shughuli nyingine za kifamilia kama mila na desturi za Kiafrika zilivyoelekeza kwa kila mwanajamii kuishi. Hata hivyo, kwa kipindi hicho cha ukoloni, bado Jeshi la jadi liliendelea kuwepo kwa kila kabila na jamii kwa vile KAR haikuwa kila sehemu ya nchi.
Baadhi ya makabila yalikuwa yamejiimarisha zaidi kiulinzi ukilinganisha na makabila mengine. Kuyataja kwa uchache ni kama vile:- Wahehe, Wanyamwezi, Wasukuma, Wamasai na Wakuria. Hawa walikuwa na mfumo wa ulinzi wa makabila yao.
Kwa mfano, kabila la Maasai walikuwa na mfumo mzuri sana wa kiulinzi. Mafunzo ya ulinzi na usalama ya kabila hilo yalikuwa yanatolewa kulingana na rika na umri wa kijana. Kadhalika, Wasukuma nao walikuwa na mfumo mzuri wa kuimarisha usalama wa kabila lao na ulinzi ambapo walikuwa wakijikusanya katika vijiji ili kutambuana na kuweka mikakati ya ulinzi katika kabila lao. Vijana walikutana kwa ajili ya kujifunza namna ya kulenga na kutupa mishale na mikuki ili kujiweka tayari kwa vita.
Jambo la msingi katika ulinzi wa jamii kabla na wakati wa ukoloni ilikuwa ni jukumu la ulinzi na usalama kuwekwa katika mikono ya kila mwanajamii. Kila mwanajamii aliyekuwa na afya njema alitakiwa kuwa mstari wa mbele kusimamia na kuhakikisha ulinzi wa kila mwanajamii ni jukumu la kila mmoja wao.
Mtemi Mirambo wa Unyanyembe aliamua kupinga ujio wa utawala wa kikoloni mwanzoni kabisa mwa karne ya 19. Uwezo na umahiri wa kijeshi wa makabila mengi hapa Tanganyika ulianza kuonekana wakati wa kupinga ukoloni kabla na baada ya Mkutano Mkuu wa Berlin 1884 hadi 1885 na mwanzoni mwa karne ya 20.
Kiongozi wa kabila la Wahehe Chifu Mkwawa alifanikiwa kupambana na utawala wa Wajerumani kwa takribani miaka mitatu, ambapo mwaka 1891 Mkwawa alishinda. Chifu Munyigumba ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa kabila la Wahehe, kati ya mwaka 1860 na 1880 aliunganisha zaidi ya koo 100 na kuwa chini ya mamlaka ya uongozi wake kitu ambacho kilimfanya Munyigumba kuonekana ndiye kiongozi mahiri wa kabila la Wahehe na alifanikiwa kutetea himaya yake kutoka kwa wavamizi wengine.
Hadi kifo chake, mwaka 1880 Munyigumba alifanikiwa kutetea kabila la Wahehe ambapo baada ya kifo chake Chifu Mkwawa alichukua nafasi na kufanikiwa kusimama imara kupinga uvamizi wa wageni. Jina ‘Mkwawa’ lilitokana na neno ’Mkwavinyika’ lenye maana ya Mteka ardhi kwa kuwa alikuwa na mfumo mzuri wa Jeshi uliomsaidia kutanua himaya yake.
Hata hivyo Chifu Mkwawa aliteua Makao Makuu yake kuwa Kalenga ambapo alijenga ngome yake yenye urefu wa kilomita 13 na ukuta kwenda juu ulikuwa na urefu wa mita 3.5 akaweza kuimarisha kambi za kijeshi na kuhamasisha mbinu nzuri za kilimo kwa watu wake na kufanikiwa kuwa na Jeshi imara ambalo lilikuwa tayari muda wote.
Kutokana na mfumo mzuri aliokuwa nao Chifu Mkwawa, aliweza kuhoji ujio wa wageni na kupigana na Wajerumani waliokuwa na silaha bora lakini aliweza kuwapa changamoto. Kutokana na upinzani wa Jeshi la Chifu Mkwawa,ilipofika Julai 1891, Kamishna wa Kijerumani Emil Von Zelewski aliongoza kikosi cha askari wa kiafrika wapatao 320 kwenda kumvamia Chifu Mkwawa, lakini alishindwa kumdhibiti kwani Jeshi la Mkwawa lilikuwa na askari 3,000 waliokuwa imara. Maafisa na askari wa Jeshi la Kijerumani wote waliuawa kwenye mapigano yaliyotokea eneo la Lugalo-Iringa.
Hata hivyo, tarehe 28 Oktoba 1894, Wajerumani chini ya Kamishna Kanali Friedrich Von Schele walipambana na Mkwawa katika ngome yake huko Kalenga, lakini kiongozi huyo alifanikiwa kutoroka. Baadaye Chifu Mkwawa alianzisha mapigano ya kuvizia hadi Julai 1898 ambapo aligundua kwamba amezungukwa na maadui na kuamua kujiua mwenyewe kabla ya kukamatwa na wakoloni wa Kijerumani.
Vita vya Majimaji ilianzishwa na makabila ya Kusini ambayo yalipinga utawala wa Kijerumani. Vita hii ilianzishwa na Wamatumbi wa eneo la Nandete katika Wilaya ya Kilwa kuanzia July 1905 hadi Agosti 1907. Kiongozi wa vita hiyo alikuwa Kinjekitile Ngwale, maarufu kama Bokero ambaye aliwapa wafuasi wake dawa ya vita ambayo aliwaambia kwamba risasi za Wajerumani zingegeuka kuwa maji.
Askari hao wa Kinjekitile walikuja kwa kasi mpya kwa kipindi hicho ambapo waliendelea kupambana na Jeshi la Wajerumani. Vita hii ilihusisha jamii mbalimbali yakiwemo makabila ya Wangindo, Wandendeule, Wabena, Wamwela na Wangoni. Vita ya Majimaji ilikuwa vita dhidi ya Wajerumani ambao walitawala Tanganyika tangu mwaka 1885 na kunyang’anya ardhi na kuvuruga maisha ya wenyeji.
Pamoja na juhudi za makabila hayo, bado Wajerumani walifanikiwa kuwashinda wapiganaji wa vita vya Majimaji kwa vile walikuwa na silaha bora. Hatimaye, mwisho wa vita ya majimaji viongozi wote wa vita hiyo walikamatwa na kunyongwa na Wajerumani.
Tanganyika ilikuwa chini ya Wajerumani baada ya Mkutano wa Berlin wa mwaka1884 hadi 1885, ulioitishwa na Chancellor Otto Von Bismark wa Ujerumani. Kipindi cha ukoloni, Wajerumani walianzisha kikosi ambacho walikiita kikosi cha kujilinda ambacho kilikuwa na Askari kati ya 2,500 na 3,000 ambao walikuwa na asili ya kiafrika na waliongozwa na Maafisa wanane wa Kijerumani japo wengine hawakuwa Maafisa. Kadiri siku zilivyokuwa zikiendelea waliendelea kuandikisha wananchi na kufikia idadi ya askari 12,000 kabla ya vita ya kwanza ya dunia. Watanganyika walioandikishwa katika Jeshi hilo waliitwa Soldat na wachache wao walifanikiwa kufikia cheo cha koplo.
Mafunzo yaliyotolewa kwa askari wa Kiafrika, yalifuata Mitaala ya Kijerumani na maelezo yake yalikuwa yakitolewa kwa lugha ya Kiswahili ambapo Dar es Salaam ilikuwa ndiyo eneo maalum kwa ajili ya kuandikisha askari wa Jeshi la kikoloni pamoja na mafunzo. Wajerumani waliviweka vikosi vyao katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Arusha, Kilimatinde Masoko, Ujiji, Bukoba, Tabora, Dar es Salaam, Mahenge, Kondoa na Mwanza.
Hata hivyo, wakati wa utawala wa Wajerumani kulikuwa na vituo mbalimbali ambavyo viliitwa DOMA kabla ya utawala wa Uingereza ambayo ilibadilishwa jina na kuitwa British Overseas Management (BOMA). BOMA zilijengwa katika wilaya kuanzia mwaka 1889 ili kudhibiti ongezeko la watu pamoja na kusimamia shughuli za kiutawala. Vituo hivi viliwekwa kwa lengo la kiulinzi na kulindwa na askari. Baada ya vita vya Chifu Mkwawa na ile ya Majimaji, maboma makubwa yalianzishwa huko Iringa, Mahenge na Songea kwa ajili ya utawala wa Wakoloni.
Wakati wa Vita Kuu ya kwanza ya Dunia mnamo 1914 hadi 1918; koloni la Tanganyika liliendelea kuwa koloni la Wajerumani kwa muda mfupi, ambapo mwaka wa kwanza wa vita vya kwanza vya dunia, Wajerumani walikuwa imara kiasi cha kupenya katika himaya za wenyeji. Kitendo cha Jeshi la Uingereza kuwavamia Wajerumani katika himaya ya Afrika ya Mashariki kilimfadhaisha Jenerali Paul Von Lettoe Vorbeck na hasa baada ya meli kutia nanga katika bandari ya Tanga, mwaka 1914.
Hata hivyo, mbinu za Kamanda huyo wa Kijerumani ziliashiria lengo la kuongeza nguvu ya msaada. Pamoja na hayo, Lettow-Vorbeck alifanya kampeni dhidi ya Waingereza na kufanikiwa kufundisha baadhi ya askari matumizi ya uwanja wa vita na eneo zuri kimapigano pamoja na namna ya kufanya shambulizi la kunuia.
Wake za askari pia walikuwa wakishirikishwa wakati wa mashambulizi. Katika harakati hizo Lettow-Vorbeck alifanikiwa kuongoza askari 15,000 wakiwemo 70 wa silaha za msaada. Askari wote hao walikuwa wanaandaliwa kukabiliana na askari wapatao 160,000 wa himaya ya Waingereza chini ya Jenerali Jan Smuts wa Afrika ya Kusini.
Hata hivyo, mwaka 1916 Smuts alifanikiwa kuteka mipaka ya Kaskazini ambayo iliwekwa chini ya Himaya ya Waingereza. Wakati huo Jeshi la Ubelgiji likiongozwa na Jenerali Charles Tombeur walifika Tabora kutoka mataifa ya Magharibi na kulazimisha kuingia mkoa wa Kagera kwa kutokea Uganda. Uwezo na nidhamu ya kimapigano ya Jeshi alilokuwa nalo Lettow-Vorbeck ulimwezesha kufanikiwa kupigana kwa muda wa miaka minne na hatimaye walishindwa rasmi mwaka 1918 kabla ya kulazimika kurudi Ulaya.
Wakati wa vita ya kwanza ya dunia askari waliokuwa wamechukuliwa Tanganyika baadaye walibadilishwa kutoka Jeshi la Wajerumani lililoshindwa na kuingizwa katika Jeshi la Waingereza lililojulikana kama Kings African Rifles (KAR). Jeshi hilo la KAR lilizidi kupanuka na kujitanua ndani ya shirikisho la Afrika ya Masharika. KAR lilikuwa na vikosi viwili ambavyo askari wake walitokea Tanganyika, Kenya na Uganda na KAR baada ya vita ilikuwa na askari kati ya 400,000 na 500,000 kutoka Afrika Mashariki.
Tanganyika ilishuhudia Waingereza kwa mara ya kwanza katika vita ya kwanza ya dunia baada ya kuishambulia Dar es Salaam kwa mzinga aina ya Mi- ser HMS Astraea na kufanikiwa kuiteka meli ya kibiashara tarehe 08 Agosti 1914. Wajerumani waliamua kuiteka bandari ya Dar es Salaam na kusababisha mapigano makali katika bandari hiyo kitu ambacho mwaka 1916 bandari iliachiwa huru.
Baada ya bandari kupata hitilafu kutokana na mapigano, wafanyabiashara wa Kijerumani na Meli yao ya SMS Konigsberg iliyokuwa inatakiwa kutia nanga Dar es Salaam ilirudi na kuingia kwa kutumia mto Rufiji kwa ajili ya kurekebisha moja ya injini zake iliyokuwa na matatizo. Baadaye tarehe 11 Julai 1915 Waingereza waligundua mahali ambapo SMS Koningsberg ilikuwepo na kuishambulia vibaya katika mto Rufiji na kuizamisha.
Wakati huo huo katika ziwa Tanganyika kulikuwa na mapigano makali kati ya wanamaji Wajerumani, Waingereza na Wabelgiji mwishoni mwa miaka ya 1915 na 1916 walikuwa wakigombea kuchukua mto. Kwa mara ya kwanza meli ya SMS Kingani ilivunjwa na kutekwa ambapo HMS foji ilibadili njia. Mara ya pili meli ya SMS Hedwing Von Wissman, SMS Graf Von Goetzen zilishambuliwa na baadae kupigwa na ndege vita za Wabelgiji na kumalizwa kabisa. Mwaka 1921 ilianza tena kuingia kwenye ukarabati ndani ya ziwa Tanganyika kuanzia mwaka 1927 na kupewa jina la MV Liemba (Graf Von Goetzen). Meli hii ya Liemba bado inafanyakazi mpaka leo hii katika ziwa Tanganyika.
Wageni walijiimarisha zaidi katika fukwe kitu ambacho kiliwafanya Wajerumani warudi nyuma kupitia ziwa Tanganyika na kuwaachia Waingereza na Wabelgiji kutawala. Wananchi wa Tanganyika walihusishwa katika mapigano ya pande zote na ndiyo waliokuwa wakiendesha hizo meli baada ya kupata mafunzo.
Kings African Rifles hapa Tanzania
Baada ya vita ya kwanza ya dunia, mamlaka ya kuongoza Tanganyika yalikuwa chini ya waingereza kwa maamuzi yaliyotolewa na Umoja wa mataifa mapema mwaka 1920 kama sharti la Ujerumani kushindwa Vita Kuu ya kwanza ya dunia. Ofisi ya Mkuu wa himaya ilianzishwa hapa nchini na kupewa jina la Himaya ya Tanganyika. Baada ya kuibuka vita ya pili ya dunia mwaka 1939 kikosi cha 6 cha KAR kilichokuwa Afrika Mashariki kiliandaliwa tayari kwa mapigano baada ya Italia kuingia vitani mwaka 1940.
Askari kutoka Tanganyika walishiriki kikamilifu katika vita kuu ya pili ya dunia kwa upande wa Uingereza. Mapigano kwa mara ya kwanza yalikuwa Somalia ambapo KAR walitembea kilomita 277 na walitumia masaa 53 kutembea kwa miguu kuelekea uwanja wa mapigano wakitokea Kenya hadi Absisinia mnamo mwaka 1940 hadi 1941 na kufanikiwa kuteka Addis Ababa ambayo ilikuwa ndiyo mji wa kivita katika historia.
Hata hivyo pamoja na kikosi cha sita cha KAR kulikuwa na kikosi cha 2 cha Zanzibar kilichohusika na huduma ya kwanza ambacho kilikuwa kikifanya kazi na kikosi cha tiba cha Afrika ya mashariki. Baadaye kikosi hicho kilienda Ceylon na kujiunga na kikosi cha 14 (XIV) ilichokuwa kimeandaliwa ili kupigana katika nchi ya Burma na Jeshi la kutoka Japan. Baada ya vita ya pili ya dunia Tanganyika iliamuriwa kuwa koloni halisi la Uingereza mnamo tarehe 13 Disemba 1946, kuanzia kipindi hicho mambo mengi ya Tanganyika yalianza kubadilika, ikiwa ni pamoja na kuanza harakati za kisiasa na uimarishaji wa Jeshi la Uingereza.
Baada ya vita ya pili ya dunia shughuli za ulinzi na usalama zilikuwa chini ya Uingereza na KAR ilizidi kujiimarisha uwepo wake hapa nchini kwa kuandikisha vijana wa Tanganyika kujiunga na KAR.
Tanganyika Rifles
Tanganyika ilipata uhuru wake tarehe 09 Disemba 1961. Katika sherehe ya uhuru serikali ya Tanganyika ilitangaza kubadili jina la Jeshi la Kings African Rifles (KAR) na kuwa Tanganyika Rifles (TR). Pamoja na jina zuri lililoakisi jina la nchi huru, TR ilibakia na mfumo ule ule wa kikoloni. Kikosi cha sita kilichokuwa katika kambi jijini Dara es Salaaam, Kiliendelea kuongozwa na Luteni Kanali Rowland Mans aliyekuwa mwingereza.
Kikosi cha pili kilichokuwa Kalewa (Mirambo Tabora) kiliendelea kuongozwa na Luteni kanali Harry Martsons mwaka 1963 ambapo alikuwa ni afisa katika Jeshi la KAR. Wakati huo huo, Kombania moja ilipelekwa Nachingwea mnamo mwaka 1963 chini ya Meja Morris Temple ambaye naye alikuwa ni mzungu kwa ajili ya kuanzisha kikosi kipya kilichopewa jina la Gonder kuwapa heshima askari kufuatia ushindi wa KAR walioupata huko Burma.
Zanzibar ilipata uhuru wake kutoka kwa Uingereza tarehe 10 Disemba 1963 baada ya uchaguzi uliokuwa na utata na ndugu Mohammed Shamte alikuwa Waziri Mkuu. Lakini Zanzibar iliendelea kuwa chini ya utawala wa Sultan Jamshid Bin Abdullah aliyeondolewa katika utawala kwa mapinduzi matukufu yaliyofanywa na wananchi wa Zanzibar tarehe 12 Januari 1964.
Mapinduzi yale yalichangiwa na waafrika walio wengi kuupinga utawala wa Sultan Abdullah. Ndiyo maana chini ya Hayati Abeid Amani Karume, waafrika walipindua utawala wa kisultan na Zanzibar ikaongozwa na Baraza la Mapinduzi hadi hii leo.
Aidha, pamoja na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar viongozi wa pande zote mbili za Tanganyika na Zanzibar walifanya maamuzi ya busara mnamo tarehe 26 Aprili 1964. Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuwaJamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa taifa moja. Kufuatia Muungano wa nchi mbili hizi ulijumuisha mambo kumi na moja kuwa ya muungano na kati ya hayo mambo ya Ulinzi yalijumuishwa katika muungano. Kwa hiyo ni dhahiri kuwa majeshi ya nchi mbili hizi yaliunganishwa rasmi tarehe 24 July 1964.
Januari 1964 ulikuwa ni mwaka muhimu sana katika historia ya siasa ya Tanzania kwani ndiyo mwaka ambao askari wa Jeshi la Tanganyika Rifles walifanya maasi tarehe 20 Januari 1964. Na ndiyo mwaka ambao TR ilivunjwa rasmi tarehe 25 januari 1964 na kupelekea Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kuzaliwa rasmi tarehe 01 Septemba 1964. Mabadiliko yaliyotokea Tanganyika yalitokea Zanzibar japo kwa namna tofauti.
Tarehe 12 Januari 1964 Jeshi la Ukombozi la Zanzibar lilizaliwa na katika mchakato wa kuunganisha nchi mbili hizo, Jeshi hilo liliungana na Tanganyika Military Force kwa muda na hatimaye kuunda Jeshi jipya lililopewa jina la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Maasi ya tarehe 20 Januari 1964 yalianzia Collito Barracks (Lugalo Dar es Salaam) na baadaye kuenea hadi Kalewa Barracks iliyokuwa Tabora. Hata hivyo maasi hayakuishia Tabora bali hata Kombania mpya iliyokuwa imepelekwa Nachingwea, kwa maandalizi ya kuanzisha kikosi kipya cha tatu hapa Tanzania nayo askari wake walijiingiza katika maasi hayo. Zipo sababu mbalimbali ambazo zimeelezwa kuwa zilikuwa ni chanzo cha maasi ya Januari 20.
Kutokana na hotuba ya Amiri Jeshi mkuu na Rais wa Tanganyika wakati huo kupitia redio ya taifa, Mwalimu Nyerere aliwaambia Wananchi kuwa Wanajeshi walikuwa na madai mbalimbali kuwa sababu za maasi ilikuwa ni pamoja na, Askari waafrika walitaka kuharakishwa kwa sera ya africanization ndani ya Jeshi la Tanganyika Rifles ili maafisa na askari wazungu waondolewe jeshini ili Wafrika maafisa na askari waongoze Jeshi lao la Tanganyika huru.
Sababu nyingine iliyokuwa kero kwa askari hawa wa TR ilielezwa kuwa ni nyongeza za mishahara. Mishahara ililipwa kwa madaraja ambapo maafisa na askari waafrika walilipwa mishahara ya chini ukilinganishwa na mishahara waliyolipwa maafisa na askari wa kizungu ilikuwa juu zaidi ya mishahara ya waafrika. Kulikuwa na madai ya askari kutaka kuboreshewa maisha na mazingira ya kazi. Hata hivyo, baada ya mazungumzo yaliyoendeshwa na Waziri wa Mambo ya nchi za nje na ulinzi Mheshimiwa Oscar Kambona, Serikali ilikubali kuongeza mishahara na kuboresha mazingira ya kazi.
Wakati maasi yakitulizwa kwa mazungumzo serikali ilifanya jitihada za kuomba msaada wa majeshi ya Uingereza kuja nchini kuzima maasi hayo. Serikali ya Tanganyika iliamua kuomba msaada kutoka serikali ya Uingereza kwa vile ingekuwa rahisi kwao kuja kwani maafisa na askari wao walikuwa wanashikiliwa na askari waliofanya maasi. Sababu nyingine ya kuwaita Uingereza kuja kumaliza mgomo, itakumbukwa kuwa bado Tanganyika Rifles ilikuwa inaongozwa na maafisa na askari viongozi wa Uingereza. Mkuu wa Majeshi ya Tanganyika wakati wa maasi alikuwa ni Brigedia Jenerali Doglous kutoka Uingereza.
Baada ya maasi kuzimwa kwa msaada wa Makomandoo wa Uingereza, viongozi wote walioshiriki kuwashawishi wenzao kushiriki katika maasi walifukuzwa Jeshini. Viongozi na vinara wa maasi wengine walifunguliwa mashitaka ya uasi. Wale maafisa na askari viongozi ambao hawakushiriki katika maasi walibakizwa jeshini kwa muda na Jeshi lilibadilishwa jina kutoka Tanganyika Rifles na kuitwa Tanganyika Military Force. Jina hilo lilidumu kwa muda mfupi hadi Jeshi jipya lilipozaliwa tarehe 01 Septemba 1964 na kupewa jina la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, jina linalotumika hadi leo.
Njia zilizotumiwa na wakoloni kuwaandikisha wanajeshi ili kuwa ni zile za kupita kijiji hadi kijiji kupima afya za vijana na kupima urefu kwa ajili ya kuwaandikisha jeshi. Lakini baada ya serikali kuvunja Jeshi la Tanganyika Rifles kutokana na maasi hayo, Amiri Jeshi mkuu na rais wa Tanganyika Mwalimu Julius Nyerere alitoa mwito kwa vijana wa TANU Youth Leaque wajiandikishe katika ofisi za TANU kwa ajili ya kuunda Jeshi jipya, Vijana wengine waliokuwa katika Jeshi la Kujenga Taifa nao waliandikishwa katika Jeshi jipya.
Tofauti na njia zilizotumiwa na wakoloni kuandikisha vijana jeshini, vijana walioandikishwa katika Jeshi jipya ni wale tu waliokuwa wazalendo na waaminifu kwa nchi yao. Vijana wanachama wa TANU walipewa umuhimu katika Jeshi jipya kwa vile chama hicho kilikuwa kimeenea nchi nzima na kilikuwa Chama cha Wazalendo.
Mafunzo kwa askari wa jeshi jipya yalianza rasmi katika kambi ya Mgulani tarehe 03 Machi 1964 hadi walipomaliza mafunzo yao ya awali tarehe 01 Septemba mwaka huohuo. Askari wapatao 1,000 walikula kiapo mbele ya Amiri Jeshi mkuu na Rais wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na Katika sherehe hizo Rais Abeid Amani Karume aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo pia alihudhuria.
Aidha, harakati za kuliimarisha Jeshi jipya zilianza kwa kasi kubwa mara tu baada ya uhuru, ili kufikia malengo ya nchi kuwa na Jeshi lake. Mafunzo kwa maafisa yalifanyika kwa muda katika nchi rafiki, kama vile Canada, Uingereza, Israeli, India, China na Pakistan. Tanzania ilitaka kujitegemea kwa kuwa na Jeshi lake lenyewe.
Kutokana na hitajio kwa maafisa na askari wenye ujuzi na waliofunzwa vizuri serikali ya Tanganyika kwa wakati ule iliamua kupeleka askari wengi nje ya nchi kufanya mafunzo ya uafisa kadiri serikali ilivyoweza. Ilikuwa ni gharama kupeleka askari nje lakini hitajio lilikuwa kubwa na nchi ililazimika kuendelea kuimarisha Jeshi kwa haraka na ilibidi kwa hali yoyote ile vijana hao wapelekwe huko ili kupata maafisa wengi kwa haraka.
Itakumbukwa kuwa kabla na baada ya kupata uhuru nchi ilikuwa na nafasi ya kupeleka afisa mwanafunzi mmoja kila mwaka nchini Uingereza kupata mafunzo, hatua ambayo ingeichukua Tanzania miaka hamsini kupata maafisa hamsini. TANU ilitumia mbinu nyingine na kupeleka vijana 15 wa TANU kufanya mafunzo ya uafisa nchini Israeli mwaka 1963.
Baada ya kuanzishwa kwa JWTZ, Jeshi liliendeleza vikosi vile vile vitatu vya askari wa miguu ingawa majina yalibadilishwa ili kulipa Jeshi taswira ya kufanana na mazingira ya Tanzania huru na kambi hizo zilizokuwa zinatumia majina ya kigeni, kuanzia wakati huo zilipewa majina ya kizalendo kama; Collito Barracks ilipewa jina Lugalo kwa ajili ya kumbukumbu ya Chifu Mkwawa wa Iringa alivyopambana na Wajerumani na kuwaua katika eneo la Lugalo. Kambi ya Kalewa Tabora ilipewa jina la Chifu Milambo kwa ajili ya kumuenzi kwa jinsi alivyosimama imara kupinga ukoloni.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.