MICHEZO JESHINI
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni moja kati ya mihimili mikuu ya taifa hili siyo tu katika maswala ya ulinzi, bali pia katika michezo. Michezo ni chombo muhimu sana katika kuiunganisha jamii. Aidha michezo huweza kuwa kielelezo na utambulisho wa Taifa kwa njia ya kutoa burudani, kujenga na kukomaza afya ya mwili na akili, kujenga nidhamu, kujitangaza kiuwezo na vipaji. Nchi inaposhiriki katika michezo ya kimataifa, michezo hulitangaza Taifa husika nje ya mipaka yake.
Katika historia ya michezo duniani, Wanajeshi walikuwa wakishiriki michezo mbalimbali tangu enzi za himaya ya kirumi. Michezo hiyo iliwajengea kujiamini na kutambuliwa na jamii zao, hivyo kuiondoa ile dhana iliyojengeka kuhusu Wanajeshi kuwa wao wapo kwa ajili ya vita na mambo ya kutumia nguvu bila akili na maarifa.
Baada ya nchi yetu kupata uhuru, Serikali mpya ya Wananchi ilitambua kuwa michezo ni sehemu ya uhai na utashi wa Taifa letu. Serikali iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na vijana mwaka 1962 ambayo ilipewa jukumu la kusimamia maendeleo ya michezo ya Nchi. Sambamba na hilo, Makao makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kuundwa upya mwaka 1964 likaunda Kurugenzi ya michezo na utamaduni ili kutekeleza sera mama ya michezo ya nchi.
Kuundwa kwa Kombania ya Michezo
Kufuatia hitajio la ushiriki wa JWTZ katika mashindano ya Kitaifa na Kimataifa mara baada ya Vita vya Kagera (1979) ziliundwa timu za Jeshi za Kundi la Vikosi na Vikosi chini ya MMJ. Aidha, kufuatia michezo ya majeshi wachezaji walioonekana kuwa na viwango vizuri waliteuliwa kuunda timu teule za jeshi na hatimaye Kombania ya Michezo ambayo ilikuwa chini ya MMJ Kombania ya utawala.
Awali kombania ya michezo iliundwa na timu za Mpira wa Kikapu na Pete. Hata hivyo ili kupanua wigo wa ushiriki baada ya mafanikio yaliyopatikana kupitia timu hizo idadi ya timu teule ziliongezeka na kuhusisha michezo ya Mpira wa wavu, miguu, mikono, riadha, ngumi na magongo.Kuundwa kwa kitivo cha utimamu wa mwili
Uwepo wa Kombania ya michezo kulisababisha hitajio la kuundwa kwa shule ya kijeshi ya mafunzo ya utimamu wa mwili na michezo, (PT and Sports Wing) hii ni kutokana na uhalisia kuwa isingelikuwa rahisi kutenganisha michezo na utimamu wa mwili kwani ni taaluma mbili zinazotegemeana. Azma ya Shule hiyo ambayo mbali na kutoa mafunzo ya Utimamu wa mwili, pia ilitoa mafunzo ya ualimu na uamuzi wa michezo mbalimbali sanjari na kusimamia ushiriki wa timu teule katika mashindano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Madhumuni ya michezo jeshini
a. Kujenga na kuimarisha afya ya mwili na akili na maisha bora kwa maafisa na wapiganaji.
b. Kujenga tabia ya ushirikiano, upendo, undugu na uzalendo miongoni mwa wanajeshi na jamii.
c. Kujenga moyo wa kishujaa, ujasiri, ukakamamvu na kujiamini.
e. Kutoa burudani kwa wananchi / jamii na hivyo kuiepusha jamii na muda wa kutenda mambo potofu.
f. Kutoa burudani, kulitambulisha na kulitangaza Taifa/ Jeshi ndani na nje ya mipaka yake.
g. Kuimarisha mahusiano kati ya Jeshi na Raia jamii kupitia michezo hivyo kuendeleza moto wa jeshi la wananchi kujitangaza kupitia michezo.
h. Kutambua, kukuza na kuendeleza vipaji vya maafisa na wapiganaji kimichezo.
m. Kujenga mahusiano mazuri kati ya Jeshi letu na majeshi mengine ndani na nje ya nchi.
Aina ya Michezo
Kurugenzi ya Utimamu wa mwili, michezo na utamaduni ndiyo yenye jukumu la kuratibu na kusimamia ushiriki wa wanajeshi katika michezo. Aidha, ushiriki wa JWTZ katika michezo umegawanyika katika makundi yafuatayo:-
a. Michezo ya Kimashindano.
Huu ni ushiriki wa wanajeshi katika michezo ya kimashindano Kitaifa na Kimataifa. Hii ni michezo inayohusisha timu au mchezaji mmoja mmoja inayochezwa ndani ya Jeshi, kitaifa au kimataifa ikiendeshwa kimashindano na ikitawaliwa na sheria za kimataifa. Aidha, ushiriki huu pia uhusisha mashindano yanayoandaliwa na mashirikisho ya Michezo ya Majeshi kutokana na Tanzania kuwa mwana chama wa mashirikisho hayo kama vile:-(1) Michezo ya Majeshi kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (Mfano kuanzia tarehe 18 Augosti 2014 hadi 30 Augosti 2014 JWTZ lilikuwa mwenyeji wa michezo hii).
(2) Shirikisho la michezo ya Majeshi ya Kanda ya Kusini Mashariki mwa Afrika (CISM ESALO-East Southern Africa Liaison Office).
(3) Shirikisho la michezo ya Majeshi la Afrika (CISM OSMA-Organization of Sports Military in Africa).
(4) Shirikisho la michezo ya majeshi ya Duniani Confederation of International Sports of Military (CISM). Mfano mwaka 1993 timu kombaini ya JWTZ ya mpira wa miguu ilishiriki katika fainali za Kombe la Dunia la Michezo ya majeshi iliyofanyika Labat- Morroco.
(5) Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA).
(a) Michezo yenye msingi wa Kijeshi ambayo siyo kuleta ushindani peke yake bali inaongeza ufanisi wa kutekeleza majukumu ya kijeshi na Taifa . Michezo kama kulenga shabaha, kuvuta kamba, Karate na Judo.Michezo ya kimashindano imegawanyika katika makundi makuu mawili :-
(b) Michezo yenye kulitangaza JWTZ nje ya Jeshi na kukuza mahusiano kati ya Jeshi na wananchi. JWTZ huwakilishwa na timu teule zilizofikia viwango vya kitaifa na kimataifa katika michezo hii. Mfano ni timu za mpira wa miguu zinazomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa za Ruvu JKT, Ruvu Shooting, Mgambo Shooting zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Timu za Kipanga FC na Hardrock za Brigedi ya Nyuki zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar. Pia zipo timu za Mpira wa Mikono, Wavu, Kikapu, Magongo, Mieleka n.k. Timu za Transit Camp, 977 KJ,82 Rangers, 44 KJ na Rhino Rangers zilishawahi kushiriki ligi kuu ya Mpira wa miguu Tanzania.
b. Michezo kwa Wote
Huu ni ushiriki wa wanajeshi wote katika michezo kama sehemu ya kazi za kila siku. Kama alivyowahi kusema Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere alipokuwa anafunga michezo ya majeshi mwaka 1978 kuwa ”Mazoezi ya mwili ni lazima kama kupumua, hivyo vijana wetu na watu wazima wajenge tabia ya kufanya mazoezi ya mwili”.
Michezo hii hufanyika mara moja au mara mbili kwa wiki vikosini kutokana na mwongozo wa MMJ. Michezo hii hulenga katika kustawisha kudumisha utimamu wa mwili na viungo wa wanajeshi wote. Makamanda wa Kamandi,Fomesheni /Shule, Vyuo na Vikosi ndiyo wasimamizi wakuu wa michezo kwa wote.
c. Ngoma na Utamaduni
Huu ni ushiriki wa J WTZ katika ngoma na utamaduni wenye lengo la kuonyesha na kudhihirisha asili ya utaifa wa nchi yetu.
.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.