Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda tarehe 09 Oktoba, 2025 alifanya ziara Visiwani Zanzibar na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa hoteli itakayokuwa na hadhi ya nyota tano.
Hoteli hiyo inayojengwa katika kambi ya Bavuai Nyuki itakuwa na ghorofa nne ambayo itakuwa na wahudumu kutoka ndani na nje ya Jeshi katika kuziunga mkono jitihada za Serikali zote mbili (Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi Zanzibar) katika kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana.
Sambamba na hilo Jenerali Mkunda alipata wasaa wa kuongea na Maafisa na Askari ambapo aliwataka kutojihusisha na shughuli za kisiasa isipokuwa Afisa na Askari wana haki ya kusikiliza sera za wanasiasa na kupiga kura ya siri kuwachagua viongozi watakaowataka wakati wa kupiga kura utakapofikia.
Aidha, alisisitiza kuwa Maafisa na Askari wanatakiwa kuwa na matumizi chanya ya mitandao ya kijamii ili kulinda amani, utulivu na kuendana na kiapo cha Jeshi. Hata hivyo alisema hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa yeyote atakayeenda kinyume na sheria, kanuni, taratibu, mila na desturi za kijeshi.
Akiagana na Maafisa na Askari waliohudhuria kikao hicho aliwaasa wakati wote kuishi katika viapo vyao na kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, utii, uhodari na weledi ili kutunza taswira chanya ya Jeshi ndani na nje ya nchi.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.