Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mh Stergomena Lawrence Tax (Mb) amefungua mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF CUP 2025) kwa msimu wa saba tangu kuanzishwa kwake. Ufunguzi huo umefanyika katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi Jijini Dar es Salaam tarehe 02 Julai 2025.
Akizungumza na Maafisa, Askari na wananchi waliohudhuria katika ufunguzi huo amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananachi Jenerali Jacob John Mkunda kwa kuendeleza michezo na kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt. Samia suhulu Hassan katika kuimarisha sekta ya michezo ambayo kwa sasa ina mchango mkubwa sana kwa Taifa letu.
Naye Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Luteni Jenerali Salum Haji Othman akimuwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda amezitaka timu zote kufuata kanuni na taratibu zinazotawala michezo na kudumisha nidhamu, Kwani kwa kufanya hivyo kutaleta ushindani na kukuza vipaji.
Mashindano haya ya CDF CUP 2025 kwa msimu huu yameboreshwa tofauti na misimu mingine ambapo baadhi ya michezo imeongezwa ambayo ni Kuogelea, karate, Golf, soka la ufukweni, Kuruka vikwazo, Vishale na mieleka.
Mashindano haya yatatamatika tarehe 13 Julai 2025 ambapo Mgeni rasmi wakati wa kufunga mashindano anatarajiwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi Jenerali Jacob John Mkunda.
Mashindano haya yatafanyika katika viwanja vya Azam complex kwa mpira wa miguu, Kambi ya Jeshi Twalipo kwa mpira wa wavu, Pete, Kikapu na Mikono (Handball), Mbweni Jkt utachezwa mchezo wa Soka la ufukweni, Msasani utachezwa mchezo wa Vishale, Uwanja wa Golf Lugalo utachezwa mchezo wa golf na Kigamboni (Kamandi ya Jeshi la Wanamaji) utafanyika mchezo wa kuogelea.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.