Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 06 Agosti 2021 amewaongoza wananchi kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Marehemu Elias John Kwandikwa katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Aidha, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Mabeyo amewaongoza Maafisa, Askari na Watumishi wa Umma wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuuaga mwili wa Marehemu Kwandikwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
Marehemu Waziri Kwandikwa alifariki Dunia tarehe 02 Agosti 2021 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.
Marehemu alizaliwa tarehe 01 Julai 1966 wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
Katika uhai wake marehemu Kwandikwa amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Kibaha, Mjumbe wa Kamati ya Siasa wilayani Kahama, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Shinyanga, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Mpaka umauti unamkuta alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Maziko yake yanatarajiwa kufanyika tarehe. 09 Agosti 2021 katika Kijiji cha Butibu, Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga
BWANA ALITOA, BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.