Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri ambapo tarehe 13 Septemba, 2021 amemuapisha Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, akichukua nafasi iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na JKT, Hayati Elias John Kwandikwa kufariki Dunia tarehe 02 Agosti, 2021. Siku moja kabla ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa Ulinzi na JKT, Mhe Rais alimteua Dkt. Tax kuwa Mbunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Dkt. Stergomena Tax anakuja na uzoefu mkubwa wa uongozi ikiwepo miaka minane aliyohudumu kama Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), nafasi aliyoitumikia tangu mwaka 2013.
Mawaziri wengine walioteuliwa na kuapishwa sambamba na Dkt. Tax katika viwanja vya Ikulu, Chamwino Dodoma ni pamoja na Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb) kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. January Yusuf Makamba (Mb) kuwa Waziri wa Nishati, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Dkt. Tax anakuwa Waziri wa 17, akiwa pia Waziri wa kwanza mwanamke kuwahi kuiongoza Wizara hii tangu ianzishwe rasmi mwaka 1962.
Akiongea baada ya kuwaapisha Mawaziri hao pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samia amesema ameamua kuvunja mwiko na fikra zilizojengeka kuwa Wizara ya Ulinzi na JKT lazima iongozwe na mwanaume kwani kwa kumteua mwanamke kuwa Waziri haendi kupiga mizinga wala kushika bunduki bali Waziri anawajibika kusimamia sera na utendaji wa rasilimali watu.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.