Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Salvatory Mabeyo jana amehitimisha mafunzo ya awali ya kijeshi kwa kozi ya kuruti kundi maalum katika Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi RTS Kihangaiko iliyopo eneo la Msata mkoani Pwani.
Jenerali Mabeyo amewapongeza Askari wapya waliohitimu mafunzo hayo na kuwataka kulitumikia Taifa kwa moyo wa uzalendo na kudumisha utii, uaminifu na uhodari katika kutekeleza majukumu ya Jeshi ili nchi iendelee kuwa salama.
Sambamba na hilo amewataka Askari wapya kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuulinda Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuepuka matumizi mabaya ya mitandao, ushabiki wa kisiasa, vikundi viovu, ulevi na lugha chafu.
Aidha, Jenerali Mabeyo aliishukuru Uongozi na Wakufunzi wa RTS Kihangaiko kwa moyo wa kujituma na kuhakikisha Askari wapya wamehitimu kwa kuzingatia viwango vya mafunzo vilivyokusudiwa.
Jenerali Mabeyo pia aliwashukuru wazazi kwa kulipa Jeshi zawadi ya nguvu kazi mpya "damu changa' na hivyo wawe na moyo wa utayari watakapoona watoto wao wanapangiwa mahali popote katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kijeshi.
Sherehe za kuhitimisha mafunzo hayo zilihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo Maafisa, Askari, Wastaafu na Wazazi wa Askari wapya waliohitimu.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.