Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Salvatory Mabeyo leo amewakaribisha nchini Maafisa na Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kundi la Tano la Ulinzi wa Amani (TANZBATT-5) lililokuwa katika nchi ya Demokrasia ya Congo (DRC)na kufanya nao mazungumzo katika Chuo Maalum cha Mafunzo ya Kijeshi kilichopo Mapinga Mkoani Pwani.
Akizungumza na Maafisa na Askari waliokuwa kwenye jukumu hilo la Ulinzi wa Amani nchini humo, alisema kuwa ni furaha kubwa na ya kipekee kupata fursa ya kuwakaribisha nyumbani na hasa kwa jukumu ambalo kwa upande wetu lilikuwa ni jaribio.
Vilevile aliwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya licha ya kuwa katika mazingira magumu na hatarishi kiusalama takribani kwa muda wa mwaka mzima wakati wa utekelezaji wa jukumu hilo.
Jenerali Mabeyo alitoa pole kwa mashambulizi ya kuvizia yaliyofanywa na baadhi ya vikundi vya waasi dhidi yao katika maeneo ya Simulike na Mayonga ambayo yalisababisha mauaji ya Askari 20 na wengine zaidi ya40 kujeruhiwa.
Mkuu huyo wa Majeshi alitoa pole kwa familia za wafiwa na kuwashukuru kwa moyo wa uvumilivu na subira na kuongeza kuwa ulikuwa ni msiba mkubwa si tu kwa Jeshibali ni kwa Taifa zima.
Aidha, Jenerali Mabeyo aliwaasa Maafisa na Askari wanaporudi vikosini watumie uzoefu walioupata kama somo na wawe mfano mzuri kwa wenzao. Aliendelea kwa kusema kuwa matukio yaliyotokea kamwe yasitutishe na kutukatisha tamaa bali yawe fundisho ili tuweze kubuni namna bora ya kukabiliana nayo na ikiwezekana kuzuia kabisa yasijtokeze tena.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.