Hafla ya kuapishwa Jenerali Venance Mabeyo ilifanyika ikulu Dar es salaam. Sambamba na kuapishwa Mkuu wa Majeshi pia ameapishwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali James Aloyce Mwakibolwa kushika wadhifa huo uliokuwa unashikiliwa na Jenerali Venance Mabeyo.
Kabla ya kuapishwa kwa viongozi hao Mhe: Rais alianza kwa kuwavalisha vyeo vipya kisha aka waapisha .Sambamba na tukio hilo Mhe: Rais na Amiri Jeshi Mkuu amemuapisha Luteni Jenerali Paul Mela(Mstaafu) kuwa balozi katika nchi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kushika nafasi iliyoachwa wazi na balozi Anthony Ngereza Cheche ambaye amestaafu.
Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Mhe: Dkt John Pombe Joseph Magufuli amesema JWTZ limeendelea kuwa na sifa nzuri kwa wananchi na mataifa mbalimbali duniani kutokana na uongozi madhubuti wa viongozi waliowahi kulitumikia jeshi, hivyo anaamini viongozi hawa wapya wataendeleza sifa hiyo kwa miaka mingi ijayo na kwamba serikali ipo pamoja na Majeshi yote katika kila hatua.
“Majeshi ya Tanzania yamekuwa na heshima kubwa si hapa nchini tu bali hata katika mataifa mengine duniani sifa za jeshi letu zinavuma. Jenerali Mwamunyange amemaliza kazi yake tunamshukuru sana, kazi yake imeonekana tunamtakia kila lakheri pamoja na familia yake” alisema Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania.
Rais na Amiri Jeshi Mkuu amesema kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Mabeyo ana changamoto ya kusimamia sera ya uchumi wa viwanda ndani ya JWTZ, na kwa kuanzia Rais alimtaka Mkuu wa Majeshi kuanza na suala la utengenezaji wa sare za Majeshi hapa nchini kwa kutumia viwanda vya ndani badala ya kuagiza kutoka nje.
Rais wa Zanzibar Mhe:Dkt Ali Mohammed Shein akiwa miongoni mwa waalikwa katika hafla hiyo aliahidi kutoa ushirikiano kwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo kwa upande wa Zanzibar. Alisema anaamini ni mtu makini kama alivyokuwa mtangulizi wake na kwamba ataendelea kuyasimamia Majeshi ya Ulinzi nchini ili yazidi kuiletea sifa Tanzania kama ilivyokuwa tangu kuasisiwa kwa majeshi hayo na Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Rais Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wote walioteuliwa na kuapishwa, amewatakia kila lakheri katika utekelezaji wa majukumu mapya ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo alijiunga na Jeshi mwaka 1979 na kupata kamisheni mwaka 1980. Amewahi kuwa mwambata Jeshi akiliwakilisha jeshi nchini Rwanda, msaidizi wa Mkuu wa Majeshi, Mkurugenzi wa idara ya usalama na utambuzi na baadaye kuwa Mkuu wa usalama na utambuzi makao Makuu ya jeshi.
Baadaye aliteuliwa kuwa mnadhimu Mkuu wa JWTZ kushika nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Jenerali Samuel Ndomba aliyestaafu kwa mujibu wa sheria mwishoni mwa mwaka 2015. Alipandishwa cheo kutoka Luteni Jenerali kuwa Jenerali na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya ulinzi Tanzania mwezi februari 2017 kushika nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali Davis Mwamunyange.
Akizungumzia uteuzi wake ,Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo amesema ameupokea na kumshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kumteua kati ya wengi na kwamba kwa kutumia mafundisho aliyoyapata kutoka kwa mtangulizi wake Jenerali Mwamunyange atatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria
Jenerali Davis Mwamunyange alijiunga na jeshi mwaka 1971 na kushika wadhifa wa Mkuu wa Majeshi mwaka 2007 kushika nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali George Marwa Waitara aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.
Katika ziara ya kuaga, Mkuu wa Majeshi mstaafu Jenerali Davis Mwamunyange amezungumzia utekelezaji wa majukumu ya kijeshi ambayo kwa uchache amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote cha uongozi wake ni mafanikio ya wanajeshi wote kwakuwa kila mmoja ndani ya JWTZ alitoa mchango wake.
Amesema hatosahau na ataendelea kuthamini ushirikiano, upendo na mchango mkubwa ambao ameupata kutoka kwa wanajeshi wote. Amesema kuwa jeshi ni familia moja iliyoshikamana kwa kuzingatia asili ya majukumu yake mengi yakiwemo mafunzo, zana na silaha zilizopo. Aliongeza kuwa kazi za jeshi ni za hatari ambazo zinataka kuaminiana, kupendana na kushirikiana kwa karibu.
“Nitaendelea kuthamini miaka yote upendo, ushirikiano na mshikamano ambao naamini mtauendeleza na kuuimarisha zaidi, sikuwahi kujuta wala kunung’unika hata siku moja kuhusu utendaji wa jeshi letu wakati wote. Wananchi wana matumaini makubwa na jeshi letu hivyo muendelee kutunza imani hiyo”amesema Jenerali Mwamunyange.
Akiongea na Ulinzi, Jenerali Mwamunyange amesema kuwa katika utumishi wake wa miaka kumi (10) akiwa Mkuu wa Majeshi jambo litakalo baki kama tukio baya zaidi kupata kutokea ni milipuko ya mabomu yaliyotokea katika kambi za jeshi za Mbagala na Gongo la Mboto “Unajua matukio mengine huwa licha ya kutokuwa ya kawaida tunafundishwa namna ya kuyakabili, lakini dharula kama ajali kama ile ya milipuko huwezi kutumia ufahamu wako wa mafunzoni, kibaya zaidi yote yalitokea nikiwa kwenye nafasi hii, kulitokea vifo, watu waliumia tulipoteza mali, kiufupi ulikuwa wakati mgumu sana kwangu kama kiongozi”alisema.
Kuhusu Jenerali Venance Mabeyo, Jenerali Davis Mwamunyange amesema ni kiongozi mwadilifu na mwenye nidhamu na kwamba amemlea tangu akiwa afisa kijana katika jeshi, hivyo ana mengi kama aliyonayo yeye kwenye masuala ya uongozi.
Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali James Aloyce Mwakibolwa ameshika wadhifa huo akitoka kuwa Mkuu wa Jeshi la nchi kavu nafasi ambayo amehudumu kwa muda wa mwaka mmoja. Alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania mwaka 1979 na kupata kamisheni mwaka 1980.
Amewahi kuwa kaimu kamanda wa brigedi ya 202, Kamanda wa Brigedi ya Majeshi ya Umoja wa Mataifa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mkuu wa Utendaji kivita na mafunzo Makao Makuu ya jeshi, Mkuu wa kamandi ya jeshi la nchi kavu na hivi karibuni amepandishwa cheo kuwa Luteni Jenerali na kuteuliwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.