Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli amezindua kiwanda cha kuchakata mahindi kinachomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale Mkoani Ruvuma.
Wakati wa uzinduzi huo Rais Dkt. Magufuli amesema kuwa JWTZ na JKT wamekuwa wakifanya kazi kwa kasi kubwa na weledi wa hali ya juu katika miradi mbalimbali pindi wanapopewa dhamana na Serikali na hata katika kazi zao wenyewe.
Akitolea mfano Rais Magufuli amesema kutokana na imani kubwa ya utendaji wa JWTZ na JKT Serikali imekuwa ikitoa zabuni za miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba na ofisi za Serikali katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, na ujenzi wa Ukuta Mirerani Mkoani Manyara ambapo Majeshi hayo yamefanya kazi hizo kwa muda mfupi na kwa ufanisi mkubwa.
Kutokana na utendaji huo wa Jeshi, Rais Dkt. Magufuli amewataka watendaji wa Sekta mbalimbali za Serikali kulikabidhi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kazi zote za dharura pale zinapojitokeza ili kuhakikisha maendeleo ya nchi yanapatikana kwa haraka.
Akiendelea kuzungumza na Makamanda na Wapiganaji waliohudhuria hafla hiyo, Rais Dkt. John Magufuli amesema kuwa amefurahishwa sana na utendaji kazi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia JWTZ na JKT kwa kazi nzuri zinazofanywa na vyombo hivyo vya ulinzi hapa nchini na nje ya nchi na kuendelea kuliletea sifa nzuri Taifa letu.
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa mbali na majukumu ya kuhakikisha mipaka ya nchi inakuwa katika hali ya usalama na amani, Jeshi limekuwa likishiriki katika shughuli za ulinzi wa amani katika nchi mbalimbali zenye migogoro kama vile Sudan, DRC, Afrika ya Kati na maeneo mengine.
Aidha,amesema kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha inapunguza utegemezi wa Bajeti na kuunga mkono Sera na jitihada za Seriakli katika kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025. Pia Waziri Mwinyi amesema kuwa Wizara yake inaendelea kujiimarisha zaidi katika maeneo ya Miundombinu (Ujenzi wa Nyumba za Watumishi), kuwa na Jeshi dogo lenye weledi, zana za kisasa ,mafunzo na mazoezi kwa Wanajeshi.
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho kilichogharimu zaidi ya shilingi Milioni 400 na chenye uwezo wa kuzalisha tani 5000 kwa mwaka umetokana na mipango ya kiubunifu na kitaalamu wa Jeshi hilo ili kuweza kufikia malengo yake ya kujiinua kimaendeleo. Aidha, amesema kuwa kiwanda hicho kitasaidia kuongeza ajira kwa wananchi wa maeneo jirani na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini. Hivyo aliwataka wananchi wa maeneo ya jirani kutoa ushirikiano kwa kiwanda hicho kwani hiyo ni mali yao kama lilivyo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Wakati huohuo Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Martin Busungu alikabidhi shilingi milioni 700 kwa Serikali ikiwa ni gawio kutoka Shirika la Uzalishaji Mali laJeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) . Kitendo hicho kimemfurahisha Mhe. Rais na kuagiza Kamati ya Bunge kufanya uchunguzi kwa Mashirika mengine na Wakuu wa Mashirika hayo na kama wameshindwa ni vema wakaachia ngazi kuwapisha wengine wayasimamie mashirika hayo kwa maslahi ya Taifa.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.