Maafisa na Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanaoshiriki Ulinzi wa Amani katika Jimbo la Darfur nchini Sudan kwa Mara ya kwanza kwa kipindi cha Miaka 10 ya Ulinzi wa Amani Jimboni humo wametumia Ndege ya Shirika la Ndege ya Serikali ya ATCL ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli katika kulifanya Shirika hilo linapiga hatua zaidi kwa maslahi ya Shirika na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita wa JWTZ Meja Jenerali Alfred Kapinga amesema Jeshi ni Taasisi inayoongozwa na Uzalendo,uadilifu, uhodari hivyo ni faraja kubwa kwa Jeshina wapiganaji kuunga mkono jitihada za Serikali katika Kuboresha Uchumi ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kuonesha uzalendo kwa vitendo kwa kutumia vitu vya nyumbani kwa maslahi mapana ya Taifa.
“ Tumekuwa tukitumia Ndege zetu za Jeshi lakini tumekuwa tukitumia Ndege za mataifa mengine kwa Mikataba kutoka Umoja wa Mataifa lakini sasa ni faraja kwani tumefanikiwa kuwashawishi Umoja wa Mataifa kutumia Ndege zetu” Alisema Meja Jenerali Kapinga.
Aidha,Meja Jenerali kapinga alisema mbali na kutumia Ndege hiyo lakini aliwaasa Maafisa na Askari hao kuhakikisha wanapeperusha vema Bendera ya Nchi na kuendelea kuitangaza kwa sifa nzuri za Utendaji Kimataifa.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Ndege la la Tanzania (ATCL),Mhandisi Ladislaus Matindi alisema ni Fursa Nzuri kwa ATCL na wanalishukuru Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kupitia kwa mkuu wa majeshi ya Ulinzikwa Mchango mkubwa kufanikisha kupata tenda hiyo.
“ Namshukuru Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo na watendaji wake kwa Uzalendo wake na kuhakikisha anafanikisha ATCL kupata fursa kwa mara ya kwanza na hii itakuwa mwanzo mzuri na tutahakikisha tunaitumia vizuri fursa hii kujitangaza zaidi Kimataifa kwa maslahi ya Nchi “ Alisema Mhandisi Matindi.
Vilevile Mhandisi Matindi aliongeza kuwa Ndege ya Dream Liner ina uwezo wa kusafiri kwa saa 12 bila kusimama, hivyo kwa kutumia saa tatu kusafiri kutoka hapa mpaka nchini Sudan ni sehemu ndogo ya Uwezo wake na ni nafasi ya kuwajaribisha watendaji wa Ndege wa ATCL katika kuhudumia safari Ndefu.
Naye Kamanda wa Kikosi cha TANZBATT- 13, Luteni Kanali Khalfan Kayage anayekwenda na Kikosi hicho alisema kuwa inawapa nguvu kupeperusha Bendera yetu kupitia Ndege na ameahidi kufanya kazi kwa Bidii kuendeleza jina na sifa nzuri ya Tanzania Kimataifa.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.