Nchi ya Zimbabwe leo imekabidhiwa Uenyekiti wa Kikundi Kazi cha Rasilimali Watu cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Arusha baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kikundi Kazi hicho Meja Jenerali Marco Gaguti kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kumaliza muda wake.
Meja Jenerali William Dube kutoka nchini Zimbabwe ndiye anayechukua nafasi hiyo kwa sasa.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kijiti hicho cha Uongozi, Meja Jenerali William Dube ameipongeza Tanzania kupitia JWTZ kwa kuweza kutekeleza majukumu yake kwa weledi na hivyo kufanikisha kukamilika kwa kazi ya kuandaa taratibu za kiutendaji zitakazotumika na Jumuiya hiyo katika majukumu yake ya ulinzi wa amani yanayoendelea nchini Msumbiji na DRC.
Aidha, Meja Jenerali William Dube amesema kuwa kupitia Jumuiya hiyo nchi wanachama wa SADC zitakuwa sehemu salama kwa kuishi bila migogoro na hivyo kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Nae Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Meja Jenerali Marco Gaguti kutoka JWTZ, amewashukuru wajumbe wote wa Kikundi Kazi cha Rasilimali Watu cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kwa ushirikiano waliompa wakati wote wa uongozi wake na kufanikisha kukamilisha jukumu alilopewa kwa weledi.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.