Mkuu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa linalotekeleza jukumu la ulinzi wa amani chini ya mpango wa amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA), Luteni Jenerali Sidiki Daniel Traore amefanya ziara ya kikazi nchini tarehe 09 May 2021, yenye lengo la kujitambulisha na kutembelea nchi ambazo zinatoa walinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Katika Ziara aliyoifanya Jijini Dar es Salaam, Jenerali Traore amekutana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Elias John Kwandikwa (MB) na kufanya nae mazungumzo ambapo alimueleza Waziri wa Ulinzi kuhusu maendeleo ya ulinzi wa amani na ushiriki wa vikundi vya Tanzania katika eneo hilo. Mkuu huyo wa Jeshi la Umoja wa Mataifa alieleza kufurahishwa na utendaji kazi wa vikundi vya Tanzania, ambapo vimekua vikiwajibika kwa weledi na kufuata taratibu na maelekezo ya Mpango wa Ulinzi wa Amani Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA).
Vile vile Jenerali Traore alikutana na kufanya mazungumzo na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Luteni Jenerali Yacoub Mohamed (Kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi) ambapo aliendelea kusifu utendaji kazi wa vikundi vya Tanzania vinavyowajibika chini ya mpango wa ulinzi wa amani Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA), na alieleza dhamira yake ya kuona nchi za Kiafrika zikiongeza ushiriki wa ulinzi wa amani (African Peacekeepers for African peace). Jenerali Traore alipata pia maelezo juu ya namna ya maandalizi ya vikundi vya walinda amani yanavyoendeshwa.
Mkuu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa (MINUSCA) alipata nafasi ya kutembelea kituo cha mafunzo ya ulinzi wa amani (PTC) ambapo akiwa kituoni hapo alipewa maelezo kubusu mafunzo na baadae kukutana na kuzungumza na walinda amani wanaojiandaa kwenda kwenye jukumu la ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Aidha, Jenerali Traore alishukuru kwa maelezo hayo na kuwatakia walinda amani hao maandalizi mema kuelekea jukumu lililo mbele yao.
Tangu Tanzania imeanza kupeleka askari wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, tayari imefikisha idadi ya vikosi vinne ambavyo vimeweza kutekeleza majukumu yake kwa lengo la kuleta amani nchini humo chini ya mwamvuli wa mpango wa amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA).
Baada ya kushuhudia mfumo wa mafunzo ya kuandaa walinzi wa amani (Pre-deployment training), Jenerali Traore alieleza kuridhishwa na viwango vya maandalizi kwa maafisa na askari wanaoshiriki ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Afrika ya kati.
Jamhuri ya Afrika ya Kati imekua katika migogoro ya mara kwa mara, hali iliyosababisha kuibuka kwa uasi uliolivuruga Taifa hilo na kuleta mpasuko wa kidinina kuendelea kwa mauaji ya kikatili dhidi ya raia wasiokua na hatia. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzani kupitia kikosi chake cha nne linaendelea kuwajibika nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kuhakikisha usalama wa raia unaimarika.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.