Mama Samia Suluhu Hassan ameapishwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibrahim Hamis Juma leo Machi 19, 2021 kuwa Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama hitajio la Kikatiba kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Tukio hilo limefanyika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Nane wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Marais wastaafu wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Mara baada ya kuapishwa Rais Samia Suluhu Hassan alipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuonesha kumtambua na kumtii kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania.
Aidha, mtangulizi wake, Hayati Rais John Pombe Magufuli aliaga dunia Jumatano Machi 17, 2021 kwa ugonjwa.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa Kifungu cha 37 (5) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa madarakani hadi mwaka 2025 wakati wa uchaguzi mwingine mkuu wa Rais na atakua na haki ya kugombea kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Mama Samia anakuwa Mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini na Afrika Mashariki.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.