Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezindua Mashindano ya Michezo ya Majeshi BAMMATA kwa mwaka wa 2025, ambayo yanafanyika mjini Zanzibar.
Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Mao Zedong na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi.
Akitoa hotuba yake, Dkt Mwinyi amewataka washiriki wote wa mashindano hayo kutambua kuwa michezo ni kielelezo cha mshikamano wa kitaifa baina ya vyombo vyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha Dkt. Mwinyi amesema "Serikali itaendelea kuunga mkono sekta ya michezo ili kukuza vipaji kwa vijana wa kitanzania sambamba na kuzijengea uwezo timu za majeshi ziweze kufanya vizuri kimataifa".
Mwisho aliwataka wachezaji wote wanaoshiriki michuano ya BAMMATA kucheza kwa nidhamu, utiifu na uhodari kama msingi wa Majeshi yote ulivyo ili kuleta burudani ya mashindano.
Nae Waziri wa Michezo wa Zanzibar Mhe. Tabia Mwita amempongeza Rais wa Zanzibar kwa ushirikiano anautoa katika sekta ya michezo ambapo mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni pamoja na ukarabati wa viwanja vya Amani Maisala na Gombani Pemba
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali John Mkunda ameishukuru Serikali ya Zanzibar kupitia Wizara ya Michezo kwa kukubali mashindano hayo kufanyika Visiwani humo.
Amesema lengo mojawapo la mashindano hayo ni "vitalu vya kukuza na kuibua vipaji."
Nae Mwenyekiti wa BAMMATA Brigedia Jenerali Said Hamis akitoa utangulizi, ameainisha viwanja vitakavyotumika ambavyo ni Amani Complex mchezo wa riadha, na viwanja vya Maisala na Mao Zedong ambapo michezo mbalimbali itachezwa.
Ameitaja michezo hiyo kuwa ni Mpira wa Pete wanawake, mpira wa miguu wanaume, mpira wa kikapu wanaume na wanawake, riadha wanawake na wanaume na shabaha kwa jinsia zote na mpira wa wavu.
Mashindano hayo ambayo yataanza kutimua vumbi kesho, yatahusisha Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama upande wa bara na visiwani kwa michezo mbalimbali
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.