Kamati ya utendaji ya ulinzi na usalama ya Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC) imekutana na kufanya kikao kuanzia tarehe 15-19 Mei 2017 jijini Dar es salaam.Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Majeshi wa nchi wanachama pamoja na wawakilishi wa Wakuu wa Majeshi kwa nchi ambazo Wakuu wa Majeshi hawakuweza kuhudhuria kutokana na sababu mbalimbali. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho.
Hata hivyo, kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha kamati ndogo ya utendaji ya Ulinzi na Usalama kilicho funguliwa na Mkuu wa mafunzo na utendaji kivita wa JWTZ Meja Jenerali Issa Nassor Mei 15 na kufungwa Mei 17 mwaka huu.Baadaye kikao kiliendelea na kuongozwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania.
Baadhi ya mambo yaliyo jadiliwa ni pamoja na hali ya Ulinzi na Usalama kwa nchi wanachama, Afrika na duaniani kwa ujumla.Vilevile masuala ya Ulinzi wa Amani katika Afrika hususani kwa wanachama wa SADC pia yalijadiliwa.
Aidha, utekelezaji wa Maazimio mbalimbali ya jumuiya hiyo yaliweza kujadiliwa wakati wa kikao hicho. Vilevile mpango kazi wa Jumuiya hiyo uliwekwa wazi ili nchi wanachama waweze kujiandaa kuutekeleza ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu ya msingi ya jumuiya hiyo kwa muda uliopangwa.
Aidha, kikao kama hicho hufanyika kila mwaka kwa mzunguko kwa nchi mwanachama.Nchi mwenyeji hutoa mwenyekiti wa kikao.Mwaka huu Tanzania ilikuwa mwenyeji.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.