Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif Ally Idd amewataka wachezaji kucheza kwa amani na upendo ili kuzidi kuitangaza vyema michezo kupitia wao katika Taifa hili.
Alisema hayo wakati wa ufunguzi wa michezo ya majeshi Tanzania BAMATTA yaliyoanza kutimua vumbi katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, huku akiwataka washiriki kuwa na Umoja kwani michezo ni afya na unajenga uhusiano mzuri.
"Kuna magonjwa ambayo mwanadamu akiyapata kuyatibu ni gharana kubwa sana, lakini kama mnafanya mazoezi kila siku magonjwa hayo hayawezi kuwapata,"alisema huku akiwataka waamuzi wa mashindano hayo kuchezesha bila kupendelea kwa kufuata Sheria husika.
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi alimshukuru Balozi Seif kwa kuipa kipaumbele michuano hii na kuja kushirikiana nao katika ufunguzi wa mashindano hayo.
Aliwataka wadhamini kuendelea na moyo huo kwa kujitolea na kusapoti mashindano haya huku akiwataka wengine kujitoa zaidi.
Aidha Dkt.Mwinyi alivipongeza vyombo vya habari kwa kujitolea sana katika kuitangaza michezo hapa nchini kwa kuwa bila wao hakuna Mwananchi ambaye angejua kama kuna tukio la aina hii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) Brigedia Jenerali Suleiman Mzee alisema mashindano hayo hudumisha na kujenga amani katika nchi yetu.
Alisema mashindano haya yameleta mafanikio makubwa ndani ya majeshi yetu na pia yamesaidia kuinua uchumi na pia uhusiano mzuri ndani na nje ya nchi.
"Michezo ni furaha ni amani na ni afya tucheze kwa furaha, kwani kupitia michezo majeshi yanazidi kuwa na ufanisi mkubwa katika utendaji kazi wao,"alisema Brigedia Mzee.
Mashindano haya ya majeshi yaliyoandaliwa na vyombo vya ulinzi na usalama hapa Nchini yamefunguliwa rasmi leo na yanatarajiwa kufikia tamati Machi 8 mwaka huu.
Aidha, mechi ya ufunguzi ya mpira wa miguu kati ya Ngome na JKT katika mashindano hayo Ngome wameibuka na ushindi magoli mawili kwa moja la JKT.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.