Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 27 Septemba, 2025 amemkabidhi Sajini taji Alphonce Simbu zawadi ya nyumba baada ya kushinda kwenye mashindano ya mbio za Dunia kwa umbali wa kilomita 42 zilizofanyika nchini Japan.
Akikabidhi zawadi hiyo kwa niaba ya Rais wakati wa Hafla ya kuwapongeza wanamichezo waliofanya vizuri katika michezo mbalimbali iliyoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) katika Hoteli ya Hyatt Regency iliyopo jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alimpongeza Sajinitaji Simbu kwa kuiwakilisha vema nchi yetu.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa Sajinitaji Simbu atakabidhiwa nyumba hiyo iliopo jijini Dodoma na Wizara ya Michezo, Utamaduni na Sanaa wakati wowote mara baada ya kukamilika.
Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya kusimamia Michezo, Utamaduni na Sanaa chini ya Mhe. Prof. Paramagamba Kabudi, imemzawadia fedha taslim kiasi cha shilingi za kitanzania Milioni Ishirini (20,000,000) kwa kuutambua mchango wake katika tasnia ya michezo hasa kupitia mchezo wa riadha kwani amekuwa akifanya vizuri mara kadhaa pale anapopata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika mashindano mbalimbali ya riadha nje ya nchi.
Nayo timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT QUEENS) ilizawadiwa kiasi cha fedha taslim za kitanzania shilingi Milioni kumi (10,000,000) kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa timu za Wanawake yaliyofanyika nchini Kenya.
Timu nyingine iliyopata zawadi ni timu ya taifa ya mpira wa Miguu kwa Watu wenye ulemavu "Tembo Warriors" baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali iliyoshiriki na kufanikiwa kuitangaza vema nchi yetu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan , amekuwa mdau mkubwa katika kukuza sekta ya michezo kwa kutoa motisha kwa wanamichezo wa michezo mbalimbali kama ule wa ngumi ijulikanayo kama 'Knockout ya Mama", kwenye mpira wa miguu kwa timu zinazowakilisha taifa katika mashindano ya kimataifa amekuwa akizizawadia timu hizo kwa kuzipatia fedha taslim kiasi cha shilingi za kitanzania milioni tano (5,000,000) kwa kila goli katika hatua za awali.
Amekwa akifanya hivyo kwa kutambua umuhimu wa sekta ya michezo kama sekta inayotoa ajira kwa vijana wengi na kwa kufanya hivyo kutatoa hamasa kwa vijana kujituma zaidi ili kufikia ndoto zao.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.