Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Magufuli leo tarehe 30 Machi 2019 amewatunuku Kamisheni Maafisa wapya 146 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Maafisa hao wametunukiwa cheo cha Luteni Usu baada ya kumaliza mafunzo yao katika Chuo cha Maafisa Wanafunzi kilichopo Monduli Jijini Arusha. Miongoni mwa maafisa waliotunukiwa kamisheni leo 140 ni wanaume na sita (6) ni Wanawake.
Rais Magufuli alisema kuwa Jeshi limekuwa likifanya vizuri katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Kitaifa na kimataifa na kuiletea sifa nzuri nchi yetu.
Aidha, aliendelea kuwapongeza Maafisa hao wapya kwa kuweza kufanya vizuri na kuonesha nidhamu nzuri kwa wakuu wao katika kipindi chote cha mafunzo licha ya kupitia katika mazingira magumu ya mafunzo ya kivita.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo amewaasa Maafisa waliotunukiwa kamisheni kuheshimu kiapo chao na kufanya kazi kwa uadilifu wakitanguliza uzalendo na utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maafisa waliotunukiwa kamisheni wanazo taaluma mbalimbali katika viwango tofauti vya elimu ikiwa ni pamoja na Shahada ya Uzamili, Shahada ya kwanza, Stashahada ya Juu na Stashahada.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.