Hivi karibuni Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya ulinzi Tanzania Mhe:Dkt John Pombe Joseph Magufuli amezindua uwanja wa ndege vita Mkoani Morogoro.
Katika hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na kijeshi, Mhe: Rais na Amiri Jeshi Mkuu ametumia fursa hiyo kumshukuru mtangulizi wake Rais mstaafu wa awamu ya nne Mhe: Dkt Jakaya Mrisho Kikwete kwa juhudi alizofanya hadi kukamilika kwa uwanja huo “Napenda kuchukuwa nafasi hii kumshukuru sana Mhe:Jakaya Kikwete kwa sababu natambua uwanja huu kwa mara ya kwanza ulijengwa katika miaka ya sabini (70) kwa msaada wa nchi ya China, kwa maana nyingine ni kuwa mazungumzo yalifanyika na marais wawili Mwl Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa China wakati huo na ulitumika kwa muda mrefu na baadaye ilionekana ipo haja ya kufanyika kwa ukarabati mkubwa, ndipo Rais wa awamu ya nne Mhe:Jakaya Kikwete na Rais wa China ndugu Ping wakafanikisha jambo hili hivyo nawashukuru sana na ninatambua mchango wao kwa hatua hii waliyofikia”
Mhe:Rais amewapongeza pia Majenerali wastaafu waliohudhuria hafla hiyo na kuwataka kuendelea kufanya hivyo kila mara kwani hali hiyo inajenga undugu na kuonesha kuheshimiana na kupendana na amewataka watumishi wote kuiga jinsi jeshi linavyoendesha shughuli mbalimbali.
Mhe: Rais ameishukuru serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa ufadhili walioutoa katika kufanikisha ukarabati huo. “Serikali ya Jamhuri ya watu wa China ni ndugu zetu wa kweli wametusaidia mambo mengi, kwa mfano kiwanda cha urafiki, TAZARA, uwanja wa Taifa na mambo mengine mengi na hapa wametoa karibu bilioni 140 kwaajili ya uwanja wa ndege vita ambao ni wa kiwango kinachokubalika wenye ambao ndege yoyote inaweza kutua, napenda Mhe:Balozi nifikishie shukrani zangu nyingi kwa Mhe:Rais Ping.” Rais amesema kazi ni nzuri na imeonekana na alitumia fursa hiyo kutoa tena shukurani kwa walioshiriki katika kufanikisha kazi hiyo wakiwemo ma engineer kutoka Jamhuri ya watu wa China, Rais pia alitumia fursa hiyo kumkumbuka mmoja wa ma engineer aliyepoteza maisha wakati wa ujenzi huo kwa kusimama kwa dakika moja.
Baada ya uzinduzi huo, likafuata onesho la ndege vita (Air show) lililochukuwa dakika thelathini kupita mbele ya Mhe: Rais na Amiri Jeshi Mkuu onesho ambalo lilihusisha ndege vita nne. Mhe: Rais na Amiri Jeshi Mkuu ameahidi kujenga barabara kutoka barabara kuu ya Morogoro (Ubena Zomozi) hadi katika uwanja wa ndege vita huo yenye urefu wa takribani kilomita kumi na mbili (12).
Waziri wa ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe: Dkt Hussein Mwinyi ametoa shukurani kwa wote walioshiriki katika kukamilisha ujenzi wa uwanja huo na miundo mbinu yake “Naomba nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa jamhuri ya watu wa China kwa kukubali kwa dhati kutoa msaada na utekelezaji mahili wa ukarabati na ujenzi wa uwanja wa ndegevita wa Ngerengere, kujitoa kwao ni ishara tosha ya kudumisha uhusiano mzuri wa kihistoria, miradi mingine tuliyosaidiwa na ndugu zetu wa China ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha ulinzi wa Taifa, ujenzi wa kituo maalum cha mafunzo Mapinga (Complehensive training centre) na kuna mradi mpya wa ujenzi wa makao Makuu mapya ya ulinzi wa Taifa tunawashukuru sana ndugu zeta wa China”
Mhe :Dkt Hussein Mwinyi amewashukuru pia viongozi wa mkoa wa Morogoro kwa kuwa mhimili Mkuu wa malighafi nyingi zilizotumika katika ukarabati na ujenzi wa uwanja huo pia amesema anatambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Jeshi la ukombozi la watu wa China (PLA) katika kuhakikisha mradi huo unakamilika. Ameupongeza pia uongozi wa JWTZ kwa mtazamo, mkakati na usimamizi ambao mara nyingi umewezesha kukamilika kwa malengo yaliyokusudiwa. Uamuzi wa kufuatilia kwa karibu ahadi na maelekezo yanayotolewa imekuwa njia madhubuti ya kufikia maendeleo yaliyopatikana kwa haraka.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Mabeyo amesema, wakati utaratibu wa kuanzisha shule ya marubani wa ndege za usafirishaji ukiendelea, shule hiyo (Ngerengere) itakuwa muongozo mzuri kufanikisha azma hiyo na kuwa uwanja huo unaweza kutumika kwa mafunzo ya marubani wa ndege za usafirishaji hivyo kuokoa fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kuwasomesha marubani hao nje ya nchi.
Amezungumzia pia umuhimu wa kuwepo kwa karakana ya ndege vita hizo ili ndege hizo kuweza kutengenezwa hapahapa nchini hivyo kupunguza gharama zinazotumika hivi sasa. Amesema anatambua mchango mkubwa wa ubalozi wa China nchini kwa kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanikisha ujenzi huo.
Pia amemshukuru Mkuu wa Majeshi mstaafu Jenerali Davis Mwamunyange kwa mchango mkubwa katika kukamilisha ukarabati na ujenzi wa uwanja huo “Shukrani na pongezi za mafaniko tunayoyaona leo hii haziwezi kukamilika bila kutambua mchango mkubwa wa Mkuu wa Majeshi mstaafu Jenerali Davis Mwamunyange, yeye ndiye alikuwa mhimili Mkuu wa ukarabati wa uwanja huu tunashukuru sana kwa jitihada zako na mapenzi makubwa uliyonayo kwa jeshi letu.Uzalendo wako wa dhati ndiyo msingi wa mafanikio tuliyonayo sasa, kuthibitisha uzalendo wake Jenerali Mwamunyange alifika kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huu siku tatu kabla ya kustaafu”.
Katika hafla hiyo Rais na Amiri Jeshi Mkuu, alikabidhi vyeti kwa wawakilishi watano kutoka serikali ya Jamhuri ya watu wa China ikiwa ni kutambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na serikali hiyo.
Uwanja huo una urefu wa kilomita tatu ambao una uwezo wa kuruhusu ndege yoyote kutua hivyo kuwa uwanja mbadala wa viwanja vya ndege nchini pindi dharula inapotokea katika viwanja hivyo.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.