Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi 386 leo tarehe 17 Aprili 2021 katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino Dodoma.
Maafisa hao wamegawanyika katika makundi matatu; Kundi la kwanza ni Maafisa Wanafunzi 143 wa Shahada ya Sayansi ya Kijeshi ambao wamefanya mafunzo kwa miaka mitatu; kundi la pili ni Maafisa Wanafunzi 226 ambao wamefanya mafunzo ya mwaka mmoja. Makundi hayo mawili yamefanya mafunzo yake katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (Tanzania Military Academy). Kundi la mwisho la Maafisa Wanafunzi 17 ambao wamefanya mafunzo yake katika nchi rafiki ambazo ni Burundi, China, India, Kenya, Marekani, Morocco na Ujerumani.
Aidha, baada ya kamisheni Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu ametunuku Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Kijeshi kwa wahitimu wa Shahada hiyo inayotolewa na Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli kwa kushirikiana na Chuo cha Uhasibu Arusha (Institute of Accountancy Arusha). Shahada hiyo inatolewa kwa mara ya kwanza na Chuo hicho tangu kuanzishwa kwake.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.