Mshindi wa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Marathoni ya Dunia yaliyofanyika Tokyo Japan Sajini Alphonce Simbu amepokelewa kishujaa na Serikali kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jijini Dar es Salaam.
Akiongea mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo Jeshini Luteni Kanali Penina Igwe amesema Sajini Simbu amekuwa shujaa wa Taifa letu la Tanzania kwa kutuletea medali ya dhahabu kwa kuwa medali hii ni ya kwanza katika nchi yetu hivyo anastahili pongezi.
Luteni Kanali Igwe aliongeza kuwa, Simbu ameliheshimisha taifa kwa ujumla na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kuleta medali ya dhahabu hapa nchini.
"Hongera sana Simbu kwa kazi nzuri uliyoifanya, leo hii Taifa na Wanamichezo wenzako wamekuja kukupokea kwa heshima kubwa hivyo tunakuombea ufanikiwe zaidi na zaidi," alisema Igwe.
Kwa upande wake Sajini Simbu, ameishukuru Serikali, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na Watanzania kumuwezesha kupata medali na kuipatia heshima Tanzania.
"Mafunzo mazuri niliyoyapata kutoka kwa kocha wangu tukiwa Jijini Arusha na malezi mazuri ya JWTZ ndio leo vimechangia kutwaa ubingwa wa Marathoni ya Dunia" alisema Simbu.
Sajini Simbu alilakiwa na mke wake Rehema Daudi Ngimba na mama yake mzazi Salome Mbua.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.