Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo anasikitika kutangaza vifo vya Maafisa wafuatao:-
Brigedia Jenerali Martin Likubuka Mwankanye (Mstaafu)
Kilichotokea mchana wa tarehe 29 Januari, 2021 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo.
Marehemu Brigedia Jenerali Martin Likubuka Mwankanye (Mstaafu) alizaliwa tarehe 01 Juni, 1955 katika Kijiji cha Nkisungu, Kata ya Rungwe, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya. Alipata Elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo Diploma in Travel Agency, kutoka Uingereza mwaka 1993; High Diploma in Business Management, kutoka Tanzania mwaka 1994; Bachelor of Arts in International Relations, kutoka Uingereza, mwaka 1999; Master of Arts in International Relation and Diplomacy, kutoka Uingereza, mwaka 2000 na National Security Study, kutoka Israel, mwaka 2009.
Marehemu alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tarehe 01 Januari, 1978. Alihudhuria kozi ya Afisa Mwanafunzi na kutunukiwa Kamisheni tarehe 19 Julai, 1980. Marehemu alipandishwa cheo kuwa Brigedia Jenerali tarehe 16 Januari, 2014 kulingana na kozi za Kijeshi alizohudhuria katika utumishi wake. Marehemu alitumikia Jeshi kwa muda wa miaka 38 na mwezi 1 hadi alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri tarehe 31 Januari, 2016.
Marehemu Brigedia Jenerali Mwankanye (Mstaafu) alitunukiwa Medali mbalimbali wakati wa utumishi wake ifuatavyo:- Vita, Miaka 20 ya JWTZ; Utumishi Mrefu Tanzania; Miaka 40 ya JWTZ; Utumishi Uliotukuka Tanzania; Miaka 50 ya JWTZ; Miaka 50 ya Muungano; Miaka 50 ya Uhuru na Nishani ya Comoro.
Katika Utumishi wake Jeshini, aliwahi kushika madaraka mbalimbali yakiwemo, Afisa Mnadhimu Makao Makuu ya Jeshi Mwaka 1981 hadi Mwaka 1986; Mkufunzi Uganda Mwaka 1986 hadi Mwaka 1989; Mkufunzi Shelisheli Mwaka 1990 hadi Mwaka 1995; Afisa Mnadhimu Makao Makuu ya Jeshi, Mwaka 2001 hadi Mwaka 2003; Mwambata Jeshi Rwanda, Mwaka 2003 hadi Mwaka 2008; Afisa Mnadhimu Makao Makuu ya Jeshi, Mwaka 2008 hadi Mwaka 2014; Mkurugenzi wa Mahusiano ya Mambo ya Nje, Makao Makuu ya Jeshi, Mwaka 2014, madaraka aliyohudumu nayo hadi anastaafu Jeshi kwa Umri tarehe 31 Januari, 2016.
Heshima za mwisho kwa marehemu zitatolewa Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo tarehe 01 Februari, 2021 Kuanzia saa 03:00 asubuhi. Baada ya hapo Mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda Kijiji cha Kibisi, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya tarehe 01 Februari 2021 na mazishi yatafanyika tarehe 02 Februari 2021. Marehemu ameacha familia.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi Amina.
Brigedia Jenerali Matata Mohamed Juma Mang’wamba (Mstaafu)
Kilichotokea Saa 11 Jioni tarehe 30 Januari, 2021 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Cardinal Lugambwa – Ukonga Jijini Dar es Salaam.
Marehemu alizaliwa mwaka, 1952 katika Kijiji cha Mkongo, Wilaya ya Rufiji, katika Mkoa wa Pwani.Marehemu alipata elimu katika ngazi mbalimbali ikwemo Elimu ya Sekondari mwaka 1968 hadi mwaka 1972 na Management Course, Tanzania mwaka 2001.
Marehemu alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tarehe 01 Juni, 1973. Alihudhuria kozi ya Afisa Mwanafunzi nchini Tanzania na kutunukiwa Kamisheni tarehe 26 Juni, 1975. Marehemu alipandishwa cheo kuwa Brigedia Jenerali tarehe 02 Septemba, 2011 kulingana na kozi za Kijeshi alizohudhuria katika utumishi wake. Marehemu alitumikia Jeshi kwa muda wa miaka 39, miezi 2 na siku 19 hadi alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri tarehe 30 Juni, 2012.
Marehemu Brigedia Jenerali Mang’wamba (Mstaafu) alitunukiwa Medali mbalimbali wakati wa utumishi wake ifuatavyo:- Vita, Miaka 20 ya JWTZ; Utumishi Mrefu Tanzania; Miaka 40 ya JWTZ na Utumishi Uliotukuka Tanzania.
Katika Utumishi wake Jeshini, aliwahi kushika madaraka mbalimbali yakiwemo, Afisa Mnadhimu, Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Anga, Mwaka 1998 hadi 1999 na Mkuu wa Shule, Shule ya Ulinzi wa Anga, Mwaka 2009, madaraka aliyohudumu nayo hadi anastaafu Jeshi kwa Umri tarehe 30 Juni 2012.
Heshima za mwisho kwa marehemu zitatolewa Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo tarehe 01 Februari, 2021 Kuanzia saa 04:00 asubuhi. Baada ya hapo Mwili wa marehemu utapelekwa Msikiti wa Miraji na baadae Mazishi katika makaburi ya Kisutu saa 07:00 Mchana. Marehemu ameacha familia.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi Amina.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.