Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo anasikitika kutangaza kifo cha Afisa Mkuu Brigedia Jenerali Stephen Ndazi Makala (Mstaafu), kilichotokea tarehe 08 Februari 2021 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo.
Marehemu alizaliwa tarehe 16 Februari 1953 katika Kijiji cha Msisi, Kata ya Ulemo, Tarafa ya Kinampanda, Wilaya ya Iramba katika Mkoa wa Singida. Alipata Elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo Shahada ya Uzamivu ya ‘Electronics’ katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1999 na ‘Defence Diplomacy’ nchini Uingereza mwaka 2003.
Marehemu alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tarehe 01 Januari 1973. Alihudhuria kozi ya Afisa Mwanafunzi hapa nchini na kutunukiwa Kamisheni mwaka 1974. Marehemu alipanda vyeo ngazi kwa ngazi hadi cheo cha Brigedia Jenerali tarehe 01 Septemba 2010. Marehemu alitumikia Jeshi kwa muda wa miaka 40, mwezi 1 na siku 14 hadi alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri tarehe 14 Februari 2013.
Brigedia Jenerali Stephen Ndazi Makala (Mstaafu) alitunukiwa Medali mbalimbali wakati wa utumishi wake ifuatavyo:- Medali ya Vita, Miaka 20 ya JWTZ; Utumishi Mrefu Tanzania; Miaka 40 ya JWTZ na Utumishi Uliotukuka Tanzania.
Katika utumishi wake Jeshini, Marehemu aliwahi kushika madaraka mbalimbali yakiwemo Afisa Mnadhimu Makao Makuu ya Jeshi mwaka 1999 hadi mwaka 2002; Afisa Mnadhimu Makao Makuu ya Kamandi ya Anga, mwaka 2002 hadi mwaka 2005; Kamanda Kikosi cha ‘Radar’ mwaka 2005 hadi mwaka 2010 na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Jamii katika Wizara ya Ulinzi na JKT mwaka 2010 madaraka aliyohudumu hadi anastaafu Utumishi Jeshini kwa umri tarehe 14 Februari 2013.
Heshima za mwisho kwa marehemu zitatolewa Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo tarehe 11 Februari 2021 kuanzia saa 03:00 asubuhi. Mwili wa marehemu utasafirishwa tarehe12 Februari 2021 kwenda Kijiji cha Ulemo, Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida kwa mazishi ambayo yatafanyika siku hiyo hiyo mnamo saa 9.00 alasiri.Marehemu ameacha mke na watoto.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.