Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi Meja Jenerali Iddi Said Nkambi kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda amepokea ujumbe kutoka Jeshi la Algeria unaoongozwa na Brigedia Jenerali Zegrour Sayed Hisham Makao Makuu ya Kamandi hiyo Upanga Jijini Dar es Salaam leo tarehe 26 Feb 2025.
Akizungumza na ujumbe huo wenye jumla ya Wajumbe 19 wakiwamo baadhi ya Wakufunzi na Wanafunzi kutoka War College Algeria amesema Uhusiano uliopo kati ya Serikali za nchi hizi mbili umezidi kuimarika siku hadi siku tangu Tanzania kupata Uhuru wake hivyo kushirikiana kwenye masuala mbalimbali kama vile biashara, diplomasia lakini zaidi katika masuala ya Ulinzi na Usalama.
Meja Jenerali Nkambi amemshukuru Mkuu wa Chuo hicho kwa kuichagua Tanzania kutembelewa na ujumbe wake na kusema kuwa ni heshima kubwa na pia itasaidia katika kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali ya Kijeshi.
Aidha, Brigedia Jenerali Zegrour naye amesema anafurahishwa sana na Uhusiano uliopo kati ya nchi hizi mbili na kwa niaba ya ujumbe huo amemshukuru Mkuu wa Kamandi ya Vikosi Chini ya Makao Makuu ya Jeshi kwa mapokezi waliyoyapata tangu kuwasili kwao.
Ujumbe huo utatembelea maeneo mbalimbali kuangalia miradi inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kituo cha Uwekezaji cha Kimataifa (EPZA), Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Chuo cha Diplomasia (CFR) vilivyopo Jijini Dar es Salaam. Aidha, Ugeni huo utatembelea vivutio vya kitalii vilivyopo Zanzibar na Bagamoyo.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.