Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Selemani Said Jafo leo amefungua Kozi Fupi Kundi la Saba ya Viongozi inayoendeshwa katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichopo Kunduchi jijini Dar es Salaam kinachomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Akifungua Kozi hiyo Waziri Jafo alisema kuwa washiriki hao wanatakiwa kuifanyia kazi kaulimbiu ya “Uzalendo na Utaifa ni Nguzo za Usalama wa Nchi” pindi watakaporudi katika vituo vyao vya kazi ili kurekebisha tabia za baadhi ya Watendaji ambao wamekuwa wakitoa taarifa za siri kwa watu wasiohusika na kuleta sintofahamu baina ya Serikali na Wananchi na hivyo kupelekea uvunjifu wa Amani nchini.
Aidha, alisisitiza kuwa ili nchi iweze kufikia Uchumi wa Kati suala la usalama ni lazima lipewe kipaumbele kwa kila mmoja wetu.
“Hatuwezi kufikia Uchumi wa Kati kama usalama wa Nchi upo mashakani na kuhisi kuwa susla hilo ni la Vyombo vya Ulinzi na Usalama peke yao, kwani tumeshuhudia mataifa mengi yakiporomoka kiuchumi kutokana na ukosefu wa Usalama” alisema Waziri Jafo.
Jumla ya Washiriki 44 kutoka Tanzania Bara na Visiwani wanatarajiwa kuhudhuria kozi hiyo inayotarajiwa kufungwa rasmi tarehe 02 Agosti 2019. Vilevile, Waziri Jafo aliutaka uongozi wa Jeshi kuongeza idadi ya Washiriki kwenye kozi hiyo ili viongozi wengi waweze kupata nafasi ya kushiriki Mafunzo hayo muhimu kwa Taifa.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Luteni Jenerali Paul Massao alimhakikishia Waziri Jafo kuwa Chuo kitaendelea kutoa Mafunzo kwa Viongozi ili Taifa liendelee kuwa Salama na kuwa na Viongozi mahili ambao watalipeleka Taifa katika kufikia Uchumi wa Kati.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.