Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) amefanya ziara Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyopo Msalato jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha kwa Maafisa, Askari na Watumishi wa Umma wanaofanyia kazi Makao Makuu ya Jeshi hilo.
Mhe. Waziri alipokelewa kwa gwaride la heshima na baadae kufanya ukaguzi kabla ya kuambatana na mwenyeji wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo kuelekea ofisini kwake.
Aidha, Mhe. Waziri alipata nafasi ya kusalimiana na Wajumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji, Wakuu wa Kamandi na Matawi wakiongozwa na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Edward Mathew Mkingule.
Baada ya mapokezi hayo Mhe. Waziri alipata wasaa wa kuzungumza mambo mbalimbali na viongozi hao wa ngazi ya juu na baadae kukutana na kada nyingine na kufanya nao mazungumzo.
Mhe. Waziri alisisitiza suala zima la ushirikiano baina ya Jeshi na Wizara kwani kwa kufanya hivyo Jeshi na Wizara kwa pamoja watafikia malengo kwa kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja changamoto zitakazokuwa zikijitokeza.
"Mimi ni mtu wa kutunga sera lakini ninyi ndio wataalamu katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku. Hivyo basi, tukiunganisha nguvu zetu kwa pamoja tutaweza kuzitatua changamoto zinazojitokeza kwa haraka na kwa usahihi" alisema Mhe. Waziri
Ziara hiyo ya Mhe. Waziri itaendelea kwa kutembeleaKamandi, Brigedi, Vikosi, Vyuo pamoja na Shule kwa lengo la kujitambulisha, kujionea utayari wa kiutendaji wa Jeshi hilo na kuzungumza na watendaji.
Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb), tarehe 10 Septemba, 2021 aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Mbunge na baadae kuteuliwa tena tarehe 13 Septemba, 2021 kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akiwa Mwanamke wa Kwanza nchini kushika nafasi hiyo tangu nchi ipate Uhurumwaka 1961.
Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb), anachukua nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Hayati John Elias Kwandikwa.
Kabla ya uteuzi wake wa kuwa Mbunge, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax, amewahi kuhudumu katika Taasisi mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.