Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) limesema litaendelea kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Rwanda ili kudumisha amani na ustawi wa maendeleo kwa nchi zote mbili.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo alipokutana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Rwanda, Jenerali Jean Bosco Kazura tarehe 10 Mei 2021 jijini Dar es Salaam.
Jenerali Mabeyo amesema nchi za Tanzania na Rwanda ni jirani na zinatakiwa kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuilinda amani iliyopo kati ya nchi hizo kwani kwa kufanya hivyo kutachochea maendeleo na kukuza uchumi.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Rwanda Jenerali Jean Kazura amelishukuru JWTZ kwa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na hivyo kuahidi kuongeza ushirikiano katika nyanja za mafunzo, ikiwa ni pamoja na kubadilishana wakufunzi ngazi za Maafisa Wanafunzi, Ukamanda na Unadhimu na Rwanda kupewa nafasi ngazi ya Chuo cha Ulinzi wa Taifa (National Dafence College). Maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na kubadilishana habari za kiutambuzi na manufaa ya pande zote.
Mbali na ushirikiano katika maeneo tajwa, Jenerali Kazura pia amesisitiza na kuahidi kuendelea kuienzi lugha adhimu ya Kiswahili kwenye Jeshi lake.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.