Mkuu wa Tawi la Ugavi na Uhandisi wa JWTZ Meja Jenerali Hawa Kodi amewataka Wataalam wa Lojistiki ndani ya JWTZ kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao wakati wa Amani na wakati wa vita ili kuviwezesha vikosi wanavyovihudumia kufanya majukumu yao bila changamoto zozote pindi wanapokuwa kwenye majukumu ya kioperesheni na kwenye mazoezi ya medani.
Meja Jenerali Kodi ameyasema hayo wakati akifunga semina ya wataalam wa Lojistiki iliyofanyika katika Shule ya Mafunzo ya Huduma Pangawe Mkoani Morogoro.
Amesisitiza kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda anaendelea kulijengea uwezo JWTZ kwa zana, mitambo na vifaa mbalimbali vya kisasa vinavyorahisisha utendaji kazi pindi wanapopewa majukumu ya kuvihudumia vikundi vinapokuwa katika operesheni mbalimbali hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi mkubwa.
Nae Mkuu wa Shule ya Huduma Pangawe Brigedia Jenerali Pasian Chausi amesema kuwa semina imeandaliwa kwa nia ya kuwajengea uwezo washiriki ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na matishio yanayoikabili Dunia kwa wakati huu.
Semina hiyo iliyofunguliwa na Mkuu wa Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo Meja Jenerali Dkt. Gabriel Muhidze imefanyika kwa muda wa wiki mbili kuanzia tarehe 11 Desemba hadi tarehe 22 Desemba mwaka huu.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.