Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi Brigedia Jenerali Iddi Nkambi amehitimisha rasmi mafunzo maalum ya kupambana na vitendo vya uhalifu vinavyojitokeza kwenye mataifa mbalimbali duniani.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Kunduchi Dar es salaam, yametolewa kwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wale wa Jeshi la Marekeni, Kamandi ya Afrika.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo, Brigedia Jenerali Nkambi amesema mafunzo hayo ni kwa ajili ya kuunganisha nguvu kati ya Tanzania na Marekani katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa kimataifa, ikiwemo ugaidi vinavyotishia ulimwengu kwa sasa.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda kikosi maalum cha JWTZ, Luteni Kanali Cliff Kulya amesema mafunzo hayo yamehusisha maafisa na askari wenye taaluma maalum na yametoa fursa kujifunza kwa pande zote mbili namna ya kukabiliana na uhalifu usiojali mipaka ya nchi.
Wakati huo huo, mwakilishi kutoka Marekani Kapteni Matt Gooh amesema mafunzo yalikuwa mazuri na yenye tija. Akaongeza kuwa "ni vyema pande zote kutumia ipasavyo uzoefu waliobadilishana katika mafunzo hayo".
Mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi julai 28, 2021 na Mkuu wa Kamandi ya Afrikawa Jeshi la Marekani, Jenerali Stephen Townsend na kuhitimishwa Septemba 10, 2021.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.