Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo anasikitika kutangaza kifo cha Afisa Mkuu Brigedia Jenerali Francis Xaiver Mbenna (Mstaafu), kilichotokea tarehe 13 Februari, 2021 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo.
Marehemu alizaliwa tarehe 31 Julai, 1930 katika Kijiji cha Nakayaya, Kata ya Mlingoti, Tarafa ya Mlingoti, Wilaya ya Tunduru katika Mkoa wa Ruvuma. Alipata Elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo Stashahada ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Hull nchini Uingereza mwaka 1960 hadi mwaka 1961.
Marehemu alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwaka 1974. Alihudhuria kozi ya Afisa Mwanafunzi hapa nchini mwaka 1974 na kutunukiwa Kamisheni tarehe 01 Julai, 1975. Marehemu alipanda vyeo ngazi kwa ngazi hadi cheo cha Brigedia Jenerali tarehe 30 Machi, 1987. Marehemu alitumikia Taifa kwa muda wa miaka 34, miezi 6 na siku moja (1) hadi alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri tarehe 30 Juni, 1988.
Brigedia Jenerali Francis Xaiver Mbenna (Mstaafu) alitunukiwa Medali mbalimbali wakati wa utumishi wake ifuatavyo:- Medali ya Vita; Miaka 20 ya JWTZ; Utumishi Mrefu Tanzania na Utumishi Uliotukuka Tanzania.
Katika utumishi wake, Marehemu aliwahi kushika madaraka mbalimbali yakiwemo Mwalimu Mkuu Songea Boys mwaka 1960 hadi 1964; Mkurugenzi wa Mafunzo na Elimu Jeshini mwaka 1985 hadi 1988 na Makamu Mwenyekiti Taifa, Chama cha Wazee (SAWATA) kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2005.
Heshima za mwisho kwa marehemu zitatolewa Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo tarehe 16 Februari, 2021 kuanzia saa 3:00 asubuhi na kuzikwa siku hiyo hiyo katika makaburi ya Temeke Wailes jijini Dar es Salaam saa 9:00 alasiri. Marehemu ameacha mke na watoto.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.