Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la nchi Kavu Meja Jenerali Anthony Chacha Sibuti leo tarehe 24 may,2022 kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi amekabidhi bendera ya Taifa kwa kikundi kinachokwenda kushiriki zoezi la Ushirikiano Imara 2022 la Majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mji wa Jinja nchini Uganda. Luteni Kanali Lucas Wambura Ryoba kamanda kikosi cha Tanzania alipokea kuashiria kwamba kikundi kipo tayari kuiwakilisha nchi katika zoezi hilo.
Zoezi la Ushirikiano Imara ni zoezi la Kijeshi lililoandaliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Majeshi ya Ulinzi, Polisi na mamlaka za kiraia (military, police & civilian component) ambapo washiriki watajikita katika maeneo manne (4) muhimu ambayo ni operesheni za ulinzi wa Amani, kukabiliana na maafa/majanga, kupambana na uharamia na kupambanana ugaidi.
Aidha zoezi hili ni la kumi na mbili (12) tangu kuanzishwa kwa mazoezi haya mwaka 2011 na washiriki kutoka Tanzania ni JWTZ, Polisi, Magereza, Zimamoto na uokoaji, Uhamiaji, Wizara ya Mambo ya Nje, Ofisi ya Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa na kituo cha kitaifa cha kupambana na Ugaidi. Lengo kuu ni kuzijengea nchi wanachama wa jumuiya katika kukabiliana na changamoto za kiusalama kwa pamoja na kudumisha ushirikiano baina ya vyombo vya Ulinzi na Usalama na wadau wengine katika operesheni za ulinzi wa Amani.
Pamoja na hayo Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu aliwaasa washiriki wa zoezi kuwa na ushirikiano miongoni mwao kama watanzania na nchi zingine na kusistiza wajifunze mambo mazuri kutoka kwa nchi zingine bila kusahau kudumisha nidhamu ,uhodari na utendaji mzuri.
Tanzania People's Defence Forces,
P.O.Box 194 Dodoma,
Street : Miyuji, Msalato
Fax : +255 26 2962123
Tel : +255 737 962 064
E-mail : ulinzimagazine@tpdf.mil.tz
Haki zote zimehifadhiwa. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.